Utumwa mamboleo unadhalilisha: haki msingi, utu na heshima ya binadamu!
Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akisikitishwa na kuguswa na mahangaiko ya watu sehemu
mbali mbali za dunia, hasa wale wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo kutokana na
kukithiri kwa biashara ya haramu ya binadamu. Baraza la Kipapa la taasisi za kisayansi
na sayansi jamii, kwa kushirikiana na Shirikisho la Madaktari Wakatoliki Duniani wameanza
semina ya kimataifa ya siku mbili, tarehe 2 Novemba na inahitimishwa tarehe 3 Novemba
2013 mjini Vatican.
Semina hii inawashirikisha wajumbe ishirini na wawili kutoka
sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni wadau wakuu katika mapambano dhidi ya biashara
haramu ya binadamu inayoendelea kushamiri sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu
unaoongozwa na kauli mbiu "Biashara haramu ya binadamu; utumwa mamboleo; udhalilishaji
wa watu na Ujumbe kutoka kwa Kristo". Wajumbe wanapania kupembua hali hali ya biashara
haramu ya binadamu ili kuibua mbinu mkakati wa kupambana na biashara hii kwa njia
za kisayansi.
Askofu Marcelo Sanchez Sorondo anasema, biashara haramu ya binadamu
ni vitendo vinavyokwenda kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu na kwamba,
vinakiuka haki msingi za binadamu. Hii ni biashara inayokuzwa na baadhi ya watu wenye
uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
wanabainisha kwamba: utumwa, ukahaba na biashara ya wanawake na watoto ni matendo
yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu na Muumba wake.
Taarifa ya Shirika
la Kazi la Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba, kati ya Mwaka 2002 hadi mwaka 2010,
zaidi ya watu millioni 20.9 wamejikuta wakitumbukizwa kwenye kazi za shuruti. Kati
yao wametelekezwa kwenye utalii wa ngono na biashara ya binadamu, kwa ajili ya kunyofolewa
baadhi ya viungo vyao, vinavyotafutwa kwa udi na ubani katika masuala ya tiba sehemu
mbali mbali za dunia.
Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, katika kipindi
cha miaka kumi ijayo, biashara haramu ya binadamu itaweza kuvuka biashara ya dawa
za kulevya na silaha duniani kutokana na faida kubwa inayopatikana kwenye biashara
hii haramu ya binadamu. Biashara ya ngono ni tatizo linaloendelea kukua na kupanuka
si tu kwa ajili ya nchi maskini duniani bali hata katika nchi tajiri na zilizoendelea
zaidi.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema,
kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu
ya binadamu, kwani hawa wanaamsha kwa mara nyingine tena madonda matakatifu ya Yesu.
Utumwa mamboleo unadhalilisha: haki msingi, utu na heshima ya binadamu.