Rais Armando Guebuza wa Msumbiji ameonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kufanya majadiliano
ya kina na Chama cha Upinzani cha RENAMO kinachoongozwa na Bwana Alfonso Dhlakama
ambaye hivi karibuni ameanza tena harakati za kutaka kurudi msituni ili kuanzisha
mapambano ya silaha, hali inayotishia amani na usalama nchini Msumbiji kwa sasa.
Rais
Guebuza anasema, licha ya tofauti za kijeshi zilizopo, lakini Serikali ya Msumbiji
bado iko wazi kwa kufanya majadiliano ili kudumisha haki, amani, utulivu, usalama
na kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Msumbiji. Chama cha RENAMO katika mikutano miwili
iliyoandaliwa na Serikali kilishindwa kupeleka wajumbe kwa madai ya kwamba, kinataka
watazamaji kutoka Jumuiya ya Kimataifa kushiriki.
Itakumbukwa kwamba, Msumbiji
ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno kunako Mwaka 1975, lakini ikajikuta ikiingia
katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyositishwa kunako mwaka 1992 kutokana na juhudi
zilizofanywa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Mkataba wa amani ukatiwa mkwaju baina
ya pande hizi mbili zilizokuwa zinapomana nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki. Rais
Geubuza anasema, RENAMO itashindwa kutambulika Kikatiba ikiwa kama itaendelea kukiuka
sheria na kanuni za nchi kuwasilisha madai na maoni yake.