2013-11-01 09:14:33

Wanachuo 468 kutunukiwa shahada MWUCE, Moshi, Kilimanjaro!


Wanafunzi 468 kutoka katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge, MWUCE, kilichoko mjini Moshi, Kilimanjaro nchini Tanzania, Jumamosi tarehe 2 Novemba 2013 wanatarajiwa kutunukiwa shahada ya kwanza, shahada ya uzamili, diploma na cheti katika masomo mbali mbali yanayotolewa Chuoni hapo.

Haya ni mahafali ya sita, tangu Chuo hiki kilipofunguliwa kama jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu nchini Tanzania. Hii ni elimu inayopania kumletea mwanadamu ukombozi kamili: kiroho na kimwili. Elimu inayotolewa Chuoni hapo inapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, mwanafunzi anapata ujuzi na maarifa katika kusoma na kufundisha; kufanya tafiti na kuzichapisha pamoja na kuendelea kushiriki katika utoaji wa huduma ndani na nje ya Tanzania.

MWUCE kinapania kuwa ni Chuo Kikuu kitakachoongoza mchakato wa kufundisha, kusoma pamoja na kufanya tafiti kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi watakaotoa huduma kwa ngazi na mahitaji mbali mbali ya Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba, wahitimu wa MUCE wanaiva barabara kitaaluma, daima wakitambua kwamba, kama raia wanawajibika kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya watu wao, kwani wanatumwa kuwa ni Mwanga wa Dunia "Lux Mundi".

Chuo pamoja na mambo mengine kinakazia: uaminifu, usawa na tunu msingi za kimaadili na utu wema. Uwajibijaki, ukweli na uwazi; umoja na ushirikiano kama timu katika utekelezaji wa mipango na mikakati ya elimu Chuoni hapo. Kila mdau wa MWUCE anafursa sawa katika kujitafutia maendeleo yake kwa kuzingatia sheria na kanuni za Chuo.







All the contents on this site are copyrighted ©.