2013-11-01 08:33:35

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Tunaendelea kama kawaida na tafakari yetu kipindi Masomo Dominika, tayari katika kalenda ya Kanisa tumekwisha safiri mpaka sasa Dominika ya 31 ya mwaka C. Mama Kanisa atuwekea Neno la Mungu, linalotuongoza kuona mwujiza wa kukutana na Bwana. RealAudioMP3

Tunaona katika somo la Injili, mtoza ushuru Zakayo, ambaye jina lake lamaanisha “Mungu anakumbuka” akiwa na mtazamo wa kina anakutana na jicho angavu, jicho la upendo na huruma, ni jicho la Bwana. Zakayo kwa jicho hilo anatafuta kumwona Bwana na si tu kumwona Bwana bali pia kumtambua na kujua Bwana ni wa namna gani, Bwana ni nani! Ili aweze kumwona Bwana na kutambua Bwana ni nani, anachangua njia ya kumwezesha kufikia ukamilifu wa nia yake. Anatambua mambo matatu: jambo la kwanza ni kwamba kuna makutano na hivi si rahisi kumwona Bwana.

Jambo la pili, yeye ni mfupi na hivi anahitaji msaada wa kuinuliwa juu, lakini sasa atainuliwa na nani? Na hivi anachagua kupanda mti wa mkuyu! na jambo la tatu ni kwamba, yeye ni mtoza ushuru karani wa Warumi, ambao hawapendwi na Wayahudi, lakini pia watoza ushuru wenyewe walikuwa na tabia ya unyanganyi na hivi walikuwa chukizo kwa watu, na hivi kuweza kumwona Bwana ilimlazimu kujitenga na makutano. Hizi ni shida ambazo anakumbana nazo Zakayo. Hata hivyo atakabiliana nazo kama inavyojionesha katika Injili na kama tulivyokwishasema. Zakayo, katika shida hizi angeweza kusema basi nitakaa katika makutano na Bwana atapita na hivi itatosheleza historia yakwamba Bwana alipita!

Lakini kwa hakika Zakayo hafanyi hilo, anatafuta si kumwona tu Bwana bali kumjua na kumtambua kwa kina. Anataka sura ya Bwana na pamoja kilichoko ndani ya moyo wa Bwana. Ni kweli kwamba uso wa Mungu na kilichoko ndani havitengani, kumbe ingetosha tu kumwona lakini, anajisikia moyoni kwamba lazima atakaswe na hivi atajiuliza swali hivi Bwana atasema nini juu yangu! Je atasema maneno makali au maneno mazuri kama afanyavyo kwa wengine waliotengwa kama tujuavyo katika Injili?
Mpendwa mwana wa Mungu kwa hakika katika sekunde hiyo Bwana atainua jicho lake angavu na la upendo upeo akimtazama Zakayo na kumwambia “shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako! Jicho la Bwana ni jicho lisilohukumu, na kunyanyasa waliowadhambi, badala yake huenda moja kwa moja na kutazama sehemu iliyo njema katika moyo wa mdhambi, sehemu ambayo kamwe dhambi haitaweza kuifikia na kuiharibu!

Kama lilivyo jina Zakayo “Mungu hukumbuka” basi ndivyo Mungu hawezi kuwasahau wadhambi kwa maana wako katika moyo wake wa milele. Yesu anakumbuka kuwa kila mtu ni mwana wa Mungu, pamoja na kwamba yawezekana kuwepo dhambi ndani mwa mtu huyo. Mpendwa msikilizaji jicho la Kristu kwa Zakayo ni sawa na jicho la Baba yake mwana mpotevu, ndilo jicho la Mungu kwetu sisi sote.

Kukutana kwa jicho la Bwana na jicho l Zakayo kunatumbusha huruma ya Mungu lakini pia kuongoka kwa Zakayo ambacho ni kielelezo cha kuongoka kwetu. Macho yetu yanaalikwa sasa kukutana na macho ya wengine na kuweza kuona ile mbegu ya utakatifu katika wao badala ya kuona mbegu ya uozo na kifo ndani mwao! Bwana anatualika kuacha maisha yetu ya zamani na kuanza maisha mapya, oneni maneno ya Zakayo, Bwana tazama nusu ya mali yangu nawapa maskini na kama nimenyang’anya nitarudisha mara nne!

Bwana ataukumbusha pia kuwa sisi sote ni ndugu na hivi tushikamane na kutafuta mbinu za kumtumikia yeye. Si hilo tu bali asema hakuna kazi au wajibu unaozuia kuingia mbinguni, hata wajibu wa kutoza ushuru, chamsingi kumtafuta Bwana katika watu kwa jicho la upendo.

Nikutakie furaha daima kumtafuta Bwana aliye mganga na mpaji wa zawadi zote za mbinguni kwa wote. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.