2013-11-01 08:29:46

Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote!


Ninakualika katika tafakari yetu tukiwakumbuka marehemu wote. Kila mwaka tarehe 2 Novemba na zaidi sana mwezi Novemba ni siku na wakati ambao Mama Kanisa anatualika kwa ajili ya kuwaombea marehemu walioko toharani.

Kwa kawaida siku zote Mama Kanisa anasali kwa ajili ya marehemu mmojammoja au kikundi lakini leo anasali kwa ajili ya Kanisa zima la wateswa lililoko toharani. Huo ndio utajiri wa kanisa linapogawa mastahili ya msalaba wa Kristu kwa wahitaji walioko safarini kuelekea mbinguni.

Mwanafalsafa John Mbiti alisema “Niko kwa sababu tuko na kwa vile tuko, kwa hiyo niko” Sentesi hii yanitafakarisha na kunisaidia kuhisi uwapo wa mwingine pembeni mwangu aliye mhitaji na hivi yaonesha hitaji la jumuiya. Katika siku ya leo Kanisa lahisi uwapo wa wahitaji ndio marehemu wote, ndio waliolala toharani wakitakaswa ili waingie mbinguni. Kanisa lahisi na kutekeleza ule muunganiko uliopo kati ya marehemu (Kanisa la wateswa), watakatifu wa mbinguni (Kanisa la washindi) na kanisa la wapiganaji ndio sisi na hivi kwa pamoja ni kanisa moja familia ya Mungu.

Fundisho tulilolisikia juu ya muunganiko wa kanisa shindi, kanisa la wateswa na kanisa la mahujaji linawekwa mbele yetu na Papa Paulo VI akisema “sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba, katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu” (KKK 962) Ndiyo kusema kuwaombea marehemu ni sehemu ya imani yetu, ni upendo kwa jirani tukiitikia injili ya Bwana ya kumsaidia aliye katika taabu, aliyemhitaji.

Kuwaombea marehemu ni kielelezo kimojawapo cha imani yetu katika ufufuko, kwa maana kama hatusadiki yakuwa Kristu alikufa na kufufuka imani yetu ni bure. Ni kutokana na msingi huo twaamini kwamba wale waliolala usingizi katika Yesu Kristu mfufuka, parapanda ya Mungu ikilia watafufuliwa kwanza nasi tuliosalia tutanyakuliwa kwa kuwafuata wao.

Kuwaombea marehemu ni jambo la thamani na la imani ambalo si la leo bali limekuwepo katika safari ya wokovu. Tunasoma daima katika kitabu cha pili cha Wamakabayo kuwa Yuda kiongozi wa Wayahudi alichanga fedha kwa kila mtu jumla drakma mbili elfu, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi. Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu. Alifanya hili kwa sababu ya imani na kama asingekuwa na imani kuwa wafu watafufuliwa ingekuwa upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. (Rej. 2Wak. 12: 43-45).

Basi ndugu yangu mpendwa, ninakualika katika msingi uleule wa imani katika ufufuko, kusali daima sala hii “raha ya milele uwape Ee Bwana na mwanga wa milele uwaangazie wapumzike kwa amani, amina”. Ni Sala ya kujenga urafiki na marehemu walioko toharani na hatimaye watakatifu wa mbinguni. Ni sala ambayo yatukumbusha wapendwa wetu ambao wengine tuliwafahamu kwa karibu na hivi yatudai wajibu wa kuomba huruma ya Mungu kwa ajili yao pasipo kukoma.

Mama Kanisa ametuwekea Misa tatu kwa ajili ya marehemu wote ili kwa njia hiyo marehemu wapate msaada wa masitahili ya Kristo kwa njia sadaka yake ya msalabani. Anataka asiwepo hata mmoja atakayekosa huruma na msaada wa Mungu. Katika Misa hizi tatu injili zagusa Heri Nane njia ya utakatifu na habari ya ufufuko wa wafu lililotumaini letu na imani yetu tunaposafiri kuelekea ukamilifu yaani uzima wa milele ambao huja baada ya kifo. Tunasali na kutumaini kuwa, kwa kifo maisha hayaondolewi ila hugeuzwa na kuwa maisha mapya, maisha makamilifu.

Basi mpendwa mwanatafakari, leo ni wakati wa kusali na kuwatembelea waliolala kule makaburini ili muunganiko katika sala ukamilishwe katika upendo unaoonekana katika maisha ya watu. Yafaa pia kufunga kidogo kwa ajili ya wapendwa wetu ili kuisimika sala yetu katika majitoleo ya Kristu mteswa na hatimaye uibuke na ushindi wa Kristo mfufuka.

Kumbukeni pia kujiombea wewe mwenyewe kwa maana kwakukumbusha kujitayarisha kwa ajili ya safari ya kugeuzwa na kuingia maisha mapya, maisha ya mbinguni. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.