2013-10-31 08:54:29

Siku kuu ya Watakatifu Wote!


Tunakuletea Habari Njema ya furaha tunapotafakari pamoja Neno la Mungu katika sherehe ya Watakatifu wote. Mama Kanisa akitaka kuhitimisha mwaka wa Kanisa kwa furaha anaona ni vema awaoneshe watoto wake lengo la maisha ya Kikristu yaani ni kuelekea maisha ya utakatifu, maisha ya milele mbinguni. RealAudioMP3
Kumbe Mama Kanisa amependa kila tarehe Mosi, Novemba ya kila mwaka, sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa zima la ulimwengu. Adhimisho hili ni mwaliko kwetu kuchuchumalia maisha yanayotimiza mapenzi ya Mungu, maisha ya ufufuko ambayo Mtume Paulo anatuambia daima akisema basi mkishafufuliwa mkayatazame yaliyo ya juu! Ni mwaliko wa kuwa Watakatifu.
Mpendwa, yafaa kutambua watakatifu ni akina nani? Watakatifu ni wale wanaokaa na Mungu katika kiti chake cha enzi kadiri tusomavyo katika kitabu cha Ufunuo. Ni marafiki wa kweli au tunaweza kusema ni marafiki wa dhati au wa kina. Ni wale ambao hula chakula pamoja na mkuu wa familia, na hivi wanafurahi pamoja na Mungu Baba huko mbinguni.
Ni wale ambao wanasadiki katika Kristu na kuishi kadiri ya mafundisho yake, urafiki ambao waliupata kwa njia ya ubatizo. Ni wale ambao Injili ilikuwa chakula chao cha kila siku walipokuwa duniani na walijikabidhi katika mikono ya Mungu na kuwa mali yake.
Mpendwa mwana wa Mungu Watakatifu ni wale walioishi heri nane mafundisho ya Kristu aliyoyatoa pale mlimani, Mt. 5:1-11 Ni wale ambao walitunza neema ya UTAKASO waliyoipokea wakati wa Ubatizo. Ni wale ambao walimpenda Mungu kwa moyo wao wote, kwa akili yao yote na kwa nguvu zao zote na kisha wakampenda jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni wale ambao katika ubinadamu wao walikubali mateso wakitambua na kujua siri ya furaha watakayoipata milele, kama ambavyo Mtakatifu Paulo asemavyo: naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha n aule utukufu utakaodhihirishwa kwetu! Rm 8:18 Sasa wanafurahia matunda ya msalaba wa Kristu. Kwa kifupi ni wale walioshika vema amri kuu ya mapendo.
Ili basi nasi tuweze kufikia hali hiyo iliyo heri na furaha upeo, somo la kwanza linaweka mwaliko kwa watu wote kuwa, ili mmoja aweze kupokea heri za milele yaani utakatifu, ni lazima kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo. Ni lazima kukinywea kikombe kimoja cha Damu Takatifu iliyo thamani ya wokovu kwa wote. Ndiyo kusema ni kuishi kwa kutimiza mapenzi ya Mungu. Kwa kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo kunamwondoa mtu katika dhiki ya dhambi na dhiki ya upungufu wa upendo mkamilifu.
Mmoja ananyakuliwa toka taabu ya ulimwengu geugeu na kuvikwa mavazi meupe ndiyo utakaso mkamilifu unaowezesha kuimba baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Huu ni wimbo wa sifa kwa Mungu ambao unaweza kuimbwa na walio wake, ndiyo watakatifu.
Katika somo la Pili Mwinjili Yohane anasema utakatifu ni maisha ambayo yanaanza katika ubatizo, na maisha haya ni fumbo lakini ambalo tunaweza kuliishi kwa furaha. Maisha haya ni zawadi toka kwa Mungu ambayo lazima kuitunza. Katika hali ya kawaida si rahisi kuuona utakatifu, lakini Yohane anasema si rahisi pia kupita bila kusikika kwa sababu ni nguvu ya Mungu katikati ya maisha yetu. Anasonga mbele akisema maisha ya utakatifu hayaendani na maisha ya wale waendao bado katika giza.
Ndiyo maana wakati wa Bwana, maadui wake hawakuweza kuona utakatifu na uchungaji wake! Hivi leo wapo bado walio katika giza ambao kazi yao ni kupingana na watumishi wa Kanisa na Kanisa zima kwa ujumla.
Mwinjili Yohane, anazungumza juu ya ukweli kwamba uko wazi sasa, na hivi Mungu hasubiri wakati ujao yaani wakati wa kufa kwetu ili kufunua ukweli huo, bali anatupatia kweli huo sasa. Hata hivyo kukamilika kwa maisha haya ni pale tutakapomwona Kristo uso kwa uso. Kwa kumwona uso kwa uso tutaweza pia kutambua asili yetu katika ukamilifu wake.
Katika Injili ya Mathayo tunapata mafundisho ya Yesu mlimani yaani Heri Nane. Bwana anaonesha njia ya kufikia utakatifu, njia ya kuishi mapenzi ya Mungu. Anaainisha namna ya kufika mbinguni, akisema, wanaheri wale walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. Wanaheri wenye upole maana watairithi nchi. Anazidi kukazia utakaso wa roho akisema heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Hizi ni baadhi ya heri nane za mlimani njia kamilifu ya kufikia utakatifu.
Kwa kuzitafakari heri nane tunaweza kusema mambo makuu mawili ni lazima katika kufikia utakatifu. Jambo la kwanza ni kujitenga na chachu ya ulimwengu. Kumbuka Bwana anasali na kusema tuko ulimwenguni lakini sisi si wa ulimwengu. Hii yamaanisha kujitenga na kile kinachopingana na injili ya Bwana, na hivi kuwa maskini wa roho.
Kumbe Mkristo anapaswa ajisikie daima kinyume na mawimbi ya ulimwengu yanayopingana na Injili. Jambo la pili ni lile la kupokea kikombe cha mateso daima na kulitangaza jina la Bwana. Mateso haya hugeuka na kuwa furaha katika maisha ya mkristo sasa anapoishi na baadaye. Mtakatifu lazima aoneshe sura ya Kristo mteswa na mwenye furaha kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Mtakatifu ni lazima amwilishe Heri Nane katika maisha yake na hivi zingae daima na kuwa kielelezo cha maisha ya upendo.
Mpendwa, hiyo ndiyo habari ya upendo mkamilifu utokao kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, na sasa unaalikwa kushiriki zawadi hii ya upendo bila kuchelewa tunapowashangilia watakatifu wa Mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.