Mshikamano wa Maaskofu kwa wananchi waliokumbwa na baa la njaa Kusini mwa Angola
Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, hivi karibuni limehitimisha
mkutano wake wa Mwaka uliokuwa unafanyika mjini Luanda. Maaskofu wamepembua na kutoa
mikakati na mipango ya Kanisa Katoliki nchini Angola, Sao Tome na Principe kwa siku
za usoni.
Maaskofu pamoja na mambo mengine wameangalia kwa kina na mapana
kuhusu baa la njaa linalowakabili wananchi wengi wanaoishi Kusini mwa Angola. Maaskofu
wanawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Angola kuonesha moyo
wa upendo na mshikamano kwa waathirika wa baa la njaa linalotishia usalama wa maisha
ya mamillioni ya watu Kusini mwa Angola. Maaskofu wanatarajia kuanzisha Kampeni ya
kuhamasisha mshikakano wa upendo na waathirika wa baa la njaa. Maaskofu wameguswa
na maendeleo yanayojitokeza katika Manispaa na miji kadhaa nchini humo.
Kwa
namna ya pekee, Maaskofu wamelaani kitendo cha kunajisi Sanamu ya Bikira kilichofanyika
hivi karibuni kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Muxima. Taarifa inaonesha kwamba,
watu sita ambao bado hawajatiwa mikononi mwa vyombo vya sheria, walifika Kanisani
hapo na kuharibu Sanamu ya Bikira Maria na baadhi ya Sanamu zilizokuwepo Madhabahuni
hapo.