2013-10-31 11:49:21

Migogoro na kinzani kati ya wakulima na wafugaji inatishia amani na utulivu Mkoani Morogoro


Shirika la Wamissionari wa Mtakatifu Francisko wa Sale linaadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu lilipofika nchini Tanzania na kuanza utume wa Uinjilishaji wa kina. Katika Maadhimisho haya, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, ameitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kabisa ili kumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama, amani na utulivu miongoni mwa Jamii hizi mbili.

Askofu Mkude ameishauri Serikali kuwahusisha viongozi wa kidini ili kuhakikisha kwamba, makundi haya mawili yanapatana na kuendelea kuishi kwa pamoja, kwa kuheshimiana. Viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa kidini, wanaweza kwa pamoja kupata suluhu ya mgogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Naye mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bwana Joel Bendera, amepongeza mchango mkubwa unaofanywa na Mashirika ya Kitawa Mkoani morogoro katika mchakato wa kuwaletea wananchi wa Morogoro maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Mashirika haya yamejikita kwa kiasi kikubwa katika huduma ya elimu, afya na maendeleo ya wanawake.

Huu ni mwendelezo wa shughuli za Uinjilishaji zilizofanywa na Wamissionari sehemu mbali mbali za Tanzania, yapata miaka 150 iliyopita. Hizi ni huduma ambazo zinatolewa bila ubaguzi wala upendeleo. Watanzania wengi wamebahatika kupata elimu yao kwa viwango mbali mbali katika shule na taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Hata leo hii kuna watanzania wengi wanaoendelea kufaidika na huduma inayotolewa na Mashirika ya Kitawa katika sekta ya afya.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amewataka Wamissionari kutokata wala kukatishwa tamaa na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza nchini Tanzania katika medani za maisha, bali wapige moyo konde wasonge mbele katika mchakato wa maboresho ya huduma ya elimu na afya kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya watanzania wengi.

Mapadre watatu wa Shirika la Mtakatifu Francsiko wa Sale kutoka India, kunako mwaka 1987 walifika nchini Tanzania kuanza maisha na utume wao miongoni mwa watanzania. Leo hii idadi yao imefikia Wamissionari 47, kumbe wanayo kila sababu ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya ulinzi na tunza yake ya Kibaba!







All the contents on this site are copyrighted ©.