Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo Tanzania kwa Mwaka 2014- 2015
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea Hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Mahusiano na Uratibu, Mheshimiwa Stephen Masato Masira (MB), akiwasilisha mapendekezo
ya mpango wa Maendeleo wa taifa 2014/15 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania likikaa kama Kamati ya mipango.
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili
liweze kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 ambayo
ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12‐2015/16).
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, sina budi kumshukuru
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye
ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Mipango kwa maelekezo yake ambayo yametuwezesha kutekeleza
majukumu ya usimamizi na uratibu wa miradi ya maendeleo. Aidha, napenda kutumia nafasi
hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa ya kuwasilisha Mapendekezo haya.
Vilevile, nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano,
maelekezo na ushauri. Tume ya Mipango itaendelea kuzingatia maoni na mapendekezo ya
Waheshimiwa Wabunge katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wa Fedha
Mhe. Dkt. William Mgimwa (Mb) kwa ushirikiano wake wakati wa maandalizi ya mapendekezo
haya. Aidha, nawashukuru Dkt. Philip Mpango, Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango pamoja
na wataalam wake, na Dkt Servacius Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha pamoja
na wataalam wake kwa ushirikiano katika kufanikisha uandaaji wa Mapendekezo ninayowasilisha.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15
ni ya nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Hivyo, Mapendekezo
haya yamezingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano vifuatavyo: (i)
Miundombinu; (ii) Kilimo; (iii) Viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuongeza
thamani; (iv) Maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi; na (v) Uendelezaji wa huduma
za utalii, biashara na fedha.
UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO
WA TAIFA 2012/13 NA ROBO YA KWANZA YA MWAKA 2013/14
Mheshimiwa
Spika, naomba nieleze kwa kifupi utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13
hususan kwa maeneo ya kitaifa ya kimkakati. Kimsingi katika utekelezaji wa Mpango
wa Maendeleo wa Taifa 2012/13, mafanikio yamepatikana katika sekta mbali mbali licha
ya kuwepo kwa changamoto kadhaa.
Mwenendo wa Uchumi kwa Mwaka 2013 Mheshimiwa Spika, taarifa za awali zinaonesha kuwa Pato halisi la Taifa
lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2013 ikilinganishwa
na ukuaji wa asilimia 6.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Sekta zilizokuwa na
viwango vikubwa vya ukuaji ni pamoja na usafiri na mawasiliano (18.4%), fedha (14.6)
na ujenzi (8.7%). Katika kipindi cha miezi tisa (9) iliyopita kasi ya mfumuko wa bei
imekuwa ikiendelea kupungua kutoka asilimia 10.9 Januari, 2013 hadi asilimia 6.1 Septemba,
2013. Kupungua kwa kasi ya upandaji bei kumetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa
mazao ya chakula hususan mpunga, mahindi na mtama.
Mheshimiwa
Spika, hali ya mwenendo wa uchumi wa Dunia sio ya kuridhisha kutokana na kupungua
kwa mahitaji na ongezeko dogo la ukuaji wa uchumi kwa Nchi Zinazoibukia Kiuchumi;
kudhoofika kwa shughuli za kiuchumi na biashara ya kifedha katika nchi za Ulaya kulikosababishwa
na mgogoro wa madeni (Euro Debt Crisis); na kupungua kwa kiwango cha ukuaji kwa nchi
ya Marekani. Kulingana na Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF ya Julai
2013, Pato la Dunia linatarajiwa kukua kwa asilimia 3.1 mwaka 2013 sawa na ilivyokuwa
katika mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukuaji wa Pato unaonesha kuanza kuimarika
na kufikia ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka
2012. Ukuaji kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nao unaonesha kuimarika
kwa nchi zote wanachama kwa kuwa na viwango vinavyoongezeka isipokuwa kwa nchi ya
Rwanda. Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na mwaka
2013 inatarajiwa kuongezeka kama ifuatavyo: Tanzania kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia
7.0; Kenya kutoka asilimia 4.7 hadi 5.9; Uganda kutoka asilimia 2.6 hadi asilimia
4.8; na Burundi kutoka asilimia 4.0 hadi asilimia 4.5. Kwa Upande wa Rwanda, kasi
ya ukuaji inatarajiwa kupungua kidogo kutoka asilimia 7.7 mwaka 2012 hadi asilimia
7.6 mwaka 2013.
Mheshimiwa Spika, Sensa ya Watu na
Makazi iliyofanyika mwaka 2012 ilionesha idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa milioni
43.6 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu milioni 43.2 mwaka 2011. Hivyo,
pato la wastani la kila mtu liliongezeka kwa asilimia 17.9 na kuwa dola za kimarekani
647 sawa na shilingi 1,025,038 mwaka 2012 ikilinganishwa na dola za Kimarekani 550
sawa na shilingi 869,436.3 mwaka 2011. Aidha, idadi ya watu Tanzania inatarajiwa
kufikia milioni 63 na kulingana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Pato la wastani
la kila mtu linatakiwa liwe limefikia dola za Kimarekani 3,000 sawa na shilingi 4,836,000
ifikapo mwaka 2025. Hivyo, ili kufikia pato hilo la wastani kwa kila mtu na kufikia
hadhi ya nchi ya kipato cha kati (dola za Kimarekani 1,036 hadi 4,085) sawa na takriban
shilingi 1,670,032 hadi 6,586,632, ni dhahiri tunahitaji msukumo mkubwa katika ukuaji
wa sekta zote hususan sekta ya kilimo yenye kuajiri watu wengi.
Mapitio
ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13
Mheshimiwa
Spika, sasa naomba nieleze kwa kifupi hali ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
Taifa 2012/13 na robo ya kwanza ya mwaka 2013/14 kwa baadhi ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la reli, mafanikio yaliyopatikana
ni pamoja na: kutandikwa kwa reli yenye urefu wa kilomita 42 na kufikisha jumla ya
kilomita 136 zilizotandikwa ikilinganishwa na kilomita 197 za reli yenye uzito wa
ratili 80 kwa yadi zilizokusudiwa katika reli ya kati; kuendelea kwa ujenzi wa madaraja
matatu ya reli, mawili kati ya Kilosa na Gulwe na moja kati ya Bahi na Kintinku; kukamilika
kwa matengenezo katika maeneo 13 kati ya stesheni ya Godegode na Gulwe na maeneo 32
yaliyopo kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe; na kufanya malipo ya awali kwa ajili
ya ununuzi wa mabehewa 34 ya breki, mabehewa 22 ya abiria na injini mpya 13 kwa ajili
ya reli ya kati. Aidha matayarisho ya kuijenga upya reli ya kati yanaendelea ambapo
upembuzi yakinifu umekamilika. Serikali ipo katika hatua ya kukamilisha upembuzi wa
kina na imeanza kumtafuta mwekezeji wa kujenga upya reli hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli ya Kikanda, hatua iliyofikiwa katika
ujenzi wa reli ya Dar es Salaam – Isaka – Kigali - Keza - Msongati (km 1,464) ni kuendelea
na kazi ya kukamilisha taarifa ya mwisho ya upembuzi wa kina inayofanywa na Mshauri
Mwelekezi Kampuni ya CANARAIL kutoka Canada. Aidha, kuhusu reli ya Tanga – Arusha
- Musoma, hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wakazi wa eneo
la Mwambani (Tanga) ili kupisha ujenzi wa sehemu ya kupanga mabehewa; na kukamilika
kwa taratibu za kumpata mtaalam mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa
kina kwa ajili ya ujenzi wa reli.
Mheshimiwa Spika,
katika kuboresha usafiri wa reli jijini Dar es Salaam, kazi zilizofanyika katika mwaka
2012/13 ni: kukarabati, kuimarisha na kupanua tuta la njia ya reli kati ya eneo la
Mnyamani na Mwananchi; kufanya matengenezo ya makutano ya njia ya reli na barabara
pamoja na kuweka alama za usalama; ujenzi wa sehemu za kupandia na kushukia abiria;
ujenzi wa sehemu za kupishania treni; na kujenga vizuizi vya magari sehemu ambazo
treni inakatisha barabara.
Mheshimiwa Spika, kwa upande
wa barabara, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: ujenzi wa kilomita 558.92 za barabara
kuu kwa kiwango cha lami ikilinganishwa na lengo la kilomita 414; na ukarabati wa
kilomita 257.53 wa barabara kuu kwa kiwango cha lami umekamilika ikilinganishwa na
lengo la kukarabati kilomita 135.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa madaraja, mafanikio ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa madaraja
ya Ruhekei (Mbinga) na Nanganga (Tunduru); na kuendelea na ujenzi wa madaraja ya
Nangoo (Mtwara), Maligisu (Mwanza), Malagarasi (Kigoma), na Mbutu (Igunga) ambao upo
katika hatua za mwisho kukamilika. Kwa upande wa daraja la Kigamboni, daraja la muda
limekamilika na kazi za ujenzi wa daraja imeanza ambapo nguzo 150 kati ya 202 zimekamilika
na kusafishwa kwa eneo la barabara zinazoingia katika daraja. Kuhusu vivuko, kazi
zilizofanyika ni pamoja na: kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV Chato (Kagera)
na ununuzi wa kivuko kipya cha Ilagala (Kigoma).
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa bandari mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa
upembuzi yakinifu wa gati nambari 1 hadi 7 katika bandari ya Dar es Salaam; kukamilika
kwa upembuzi yakinifu na kusainiwa kwa makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Watu wa China kwa ajili ya ujenzi wa bandari
ya Mbegani (Bagamoyo); kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kutangaza mradi wa bandari
ya Mwambani (Tanga) ili kupata wawekezaji wa kuendeleza bandari kwa ubia. Kuhusu bandari
kavu Kisarawe, hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa mchakato wa zabuni kwa ajili ya
upembuzi yakinifu awamu ya pili na Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kukamilisha
taratibu za kupata kibali kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi cha
kutenga eneo la ekari 1,760 badala ya ekari 1,468 za awali.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa miradi ya maji safi na majitaka, mafanikio yaliyopatikana ni
pamoja na: kusimikwa kwa mitambo ya umeme na mashine za kusukuma na kusafisha maji
katika mradi wa Ruvu Chini na kutandazwa kwa mabomba katika eneo la kilomita 17.1
kati ya kilomita 55 zilizokusudiwa. Kwa upande wa mradi wa maji Ruvu Juu, ripoti ya
usanifu kwa ajili ya kutandaza bomba kuu kutoka mtamboni hadi Kibamba, na ujenzi wa
tanki jipya eneo la Kibamba, umekamilika Novemba, 2012 na kukamilika kwa taratibu
za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi, Agosti, 2013. Aidha, idadi ya wakazi wa
vijijini wanaopata maji safi imeongezeka kutoka watumiaji milioni 20.6 mwaka 2011
hadi milioni 22.29 mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika,
katika eneo la nishati, kazi zilizofanyika katika mradi wa Bomba la Gesi (Mtwara -
Dar es Salaam) ni: kukamilika kwa ulipaji wa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 6.86
kwa wananchi, kupatikana kwa cheti cha mazingira tangu mwezi Aprili 2012, kuwasili
kwa mabomba ya gesi 20,491 yenye uwezo wa kujenga kilomita 243.86 na kutandazwa kwa
mabomba yenye urefu wa kilomita 108 ambapo mabomba yenye urefu wa kilomita 25.8 yameunganishwa.
Mheshimiwa Spika, katika mradi wa mtambo wa kufua
umeme Kinyerezi I (MW 150) hatua iliyofikiwa ni kuingia mkataba kati ya Serikali na
Mkandarasi (M/s Jacobsen Electro AS) kutoka Norway na mshauri wa mradi (M/s Lahmeyer)
kutoka Ujerumani. Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuboreshwa kwa miundombinu ya
usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam katika vituo vya Buguruni, katikati ya jiji,
Kariakoo, Kipawa, Mbagala, Mbezi, Oysterbay na Ubungo kwa kufungwa kwa transfoma zenye
uwezo wa MVA 15 kwa kila kituo.
Mheshimiwa Spika,
mafanikio yaliyopatikana katika miradi ya umeme vijijini ni pamoja na: kupeleka umeme
Makao Makuu ya Wilaya za Namtumbo, Nyang’hwale na Nkasi; kupata Mkandarasi wa kupeleka
umeme makao makuu ya wilaya za Bukombe na Mbogwe; kukamilisha tathmini ya zabuni za
kuwapata wakandarasi wa kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme
Vijijini; kukamilisha ujenzi wa kilomita 24.78 kati ya 47.53 za njia za usambazaji
umeme na kufunga transfoma 7 kati ya 24 mkoani Mtwara na kuunganisha umeme kwa wateja
277; na kukamilisha ujenzi wa jumla ya kilomita 11.28 kati ya 28.20 za njia ya umeme
ya msongo wa kV 33 na kV 11 katika mkoa wa Lindi. Aidha, ujenzi wa kilomita 59.5 kati
ya 72.3 za njia ya umeme ya msongo wa kV 0.4 mkoani Lindi umekamilika na transfoma
5 kati ya 25 zimefungwa, na wateja 132 wameunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kilimo, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja
na kutambua na kuhakiki mashamba yenye ukubwa hekta 334,538 kwa ajili ya uwekezaji
katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Rufiji, Kagera, Kilombero na Malagarasi ambapo
hekta 85,000 zimepata hatimiliki. Aidha, kazi ya kupima maeneo inaendelea katika bonde
la Rufiji - Mkongo Block ambapo jumla ya hekta 5,551 zimepimwa. Kwa upande wa miradi
ya Ukanda wa SAGCOT, hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa asilimia 40 ya ujenzi wa
banio katika mradi wa umwagiliaji – Itete, Morogoro (Hekta 1,000). Aidha, katika
miradi ya umwagiliaji ya Mpanga –Ngalimila, Morogoro (Hekta 31,500), Sonjo – Kilombero
(Hekta 1,340) na Lupilo, Morogoro (Hekta 4,000), kazi ya upembuzi yakinifu imekamilika
na kazi za usanifu na kuandaa michoro ya skimu inaendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula,
ujenzi wa ghala katika kanda ya Songea lenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 upo katika
hatua za mwisho. Aidha, michoro kwa ajili ya ujenzi wa ghala la Mbozi na ghala jingine
Songea imekamilika. Vile vile, majadiliano kati ya Serikali na benki ya Exim ya China
yameanza kwa ajili ya kupata mkopo wa kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo
wa kuhifadhi jumla ya tani 160,000 katika kanda za Kipawa, Makambako, Sumbawanga,
Songea, Shinyanga, Arusha na Dodoma.
Mheshimiwa
Spika, Katika sekta ya viwanda, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilisha
uchorongaji wa mashimo 40 yenye jumla ya urefu wa mita 8,000 kwa ajili ya kuhakiki
wingi wa chuma katika eneo la Liganga; na kukamilisha tathmini ya eneo la Kurasini
ekari 60 lenye thamani ya shilingi bilioni 94.1 Mei, 2013 na kulipa fidia ekari 19.6
kwa kaya 278. Aidha, ulipaji fidia ya kiasi cha shillingi bilioni 16.9 kwa eneo la
Bagamoyo ulifanyika mwaka 2011/12 na mwaka 2012/13 kwa hekta 1,600 kati ya 5,700 zilizofanyiwa
tathmini ya shillingi bilioni 58.8 mwaka 2011. Kwa upande wa Kigoma, malipo ya shilingi
bilioni 1.5 kwa hekta 3,000 kati ya hekta 20,000 yalifanyika mwaka 2011/12. Mchakato
wa kupata fedha za kumalizia kulipa fidia katika eneo la mradi Bagamoyo na Kigoma
unaendelea kwa mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
ujenzi wa kiwanda cha Viuadudu Kibaha, hatua iliyofikiwa ni ujenzi wa majengo mawili
ya kiwanda; usanifu wa kina na kuanza ufungaji wa mitambo. Kiwanda hiki tayari kimezinduliwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Oktoba, 2013. Kwa upande wa mradi wa Magadi Soda- Bonde la Engaruka (Arusha), kazi
ya kuchoronga mashimo 12 kwa ajili ya kuhakiki wingi na ubora wa magadi imekamilika,
ambapo imebainika kuwa eneo la Engaruka lina magadi yenye mita za ujazo bilioni 4.68
kiasi ambacho ni kikubwa kutosheleza uchimbaji magadi soda kwa zaidi ya miaka 400.
Upatikanaji wa magadi soda utasaidia katika viwanda vya madawa, sabuni, nguo, rangi,
na viwanda vya kuchakata chuma. Kwa sasa Serikali inaendelea na tafiti za kubaini
tabia za ndege aina ya Flamingo ili kuendana na matakwa ya kimazingira, ujenzi wa
miundombinu na kutafiti teknolojia bora za uchimbaji wa magadi soda.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa rasilimali watu, mafanikio yaliyopatikana
hadi Juni, 2013 ni pamoja na: wataalamu wapatao 374 wameendelea kugharimiwa na Serikali
katika nyanja maalum za gesi, mafuta, chuma, urani na madini mengine, na nyanja nyingine
muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Kati ya hao, 261 ni wa shahada ya uzamili
na 133, shahada ya uzamivu na wanasoma katika vyuo vikuu sita vya umma ambavyo ni
Dar-es Salaam, Sokoine, Muhimbili, Mzumbe, Ardhi na Nelson Mandela.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kugharamia miradi ya utafiti
hapa nchini ikiwa ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya utafiti, kutengeneza
mitambo na vipuri. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilisha ukarabati wa
matrekta 11 kati ya 14 ambao umefanywa na CAMARTEC; kukamilika kwa matengenezo ya
vipuri vya treni, reli, na trekta ndogo za mikono (power tiller) yaliyofanywa na
Taasisi ya Tanzania Automotive Technology Centre (TATC) iliyopo Kibaha; na kuendeleza
ubunifu na uendelezaji wa mashine mbalimbali kwa ajili ya usindikaji mazao.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la huduma za fedha, mafanikio yaliyopatikana
ni kuundwa kwa bodi ya wakurugenzi, na kuanza kuajiri maafisa waandamizi na kuongeza
mtaji wa Benki ya Kilimo kufikia shilingi bilioni 90; kuongeza mtaji wa shilingi bilioni
50 kwa Benki ya Rasilimali Tanzania na kufikia shilingi bilioni 142; na kuongeza mtaji
wa shilingi bilioni 1.1 kwa Benki ya Wanawake Tanzania na kufikia shilingi bilioni
8.2.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu malengo
na hatua ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2012/13 na robo ya
kwanza kwa mwaka 2013/14 kwa baadhi ya maeneo yakijumuisha mafanikio yaliyopatikana
kwa upande wa sekta binafsi yapo katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo
wa Taifa 2014/15 (Sura ya pili).
Changamoto na Hatua Zilizochukuliwa
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2012/13,
pamoja na mafanikio yaliyopatikana, kumekuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja
na:- ufinyu wa rasilimali fedha hususan upatikanaji wa mikopo ya kugharamia miradi;
taratibu za tathmini ya fidia na ulipaji fidia kwa wakati; upatikanaji wa ardhi iliyopimwa
kwa ajili ya uwekezaji; upatikanaji wa huduma wezeshi hususan barabara, maji na umeme
katika maeneo ya miradi; na madeni ya miaka iliyopita kwa baadhi ya miradi.
Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo
ni pamoja na: kuendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato; kuandaa mwongozo
wa andiko la miradi kwa ajili ya kuziwezesha wizara kuandaa miradi itakayokidhi vigezo
vya mikopo; kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi chini ya President’s
Delivery Bureau; na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza
ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
MAENEO
MUHIMU YA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2014/15
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuelekeza fedha za maendeleo kwenye
miradi michache ya kitaifa ya kimkakati na yenye kuleta matokeo makubwa ili kuchochea
uwekezaji wa sekta binafsi, na hivyo kuongeza ajira, uzalishaji hususan katika sekta
ya kilimo kwa lengo la kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei, kuimarisha ushindani wa
kiuchumi, kuongeza mauzo nje ya nchi na kupunguza umasikini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia fursa za kikanda na dunia, jitihada za
ziada zinahitajika ili kuhakikisha kuwa zinaleta matokeo chanya na kwa haraka. Hivyo,
inapendekezwa kuwa masuala muhimu yafuatayo yazingatiwe katika kuandaa Mpango wa Maendeleo
wa Taifa 2014/15:
Kudumisha amani na utawala
bora kama msingi muhimu wa kuwezesha uzalishaji mali, uwekezaji, ukuaji wa uchumi
na maendeleo ya kiuchumi na kijamii; Ukuaji uchumi unakuwa shirikishi ili kuondoa
tofauti za kipato na kupunguza umaskini; Kuongeza tija katika kilimo hususan mazao
yenye thamani kubwa (high value crops); Ubunifu na maendeleo ya teknolojia kuharakisha
maendeleo ya kiuchumi na kijamii; Masoko kwa bidhaa za ndani na vyanzo vipya vya
uwekezaji katika uchumi wa Kikanda na Dunia vinatumika vizuri; Kujenga uwezo wa
kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi; Kujenga uwezo wa kutumia
vizuri mapato yatakayotokana na gesi asilia na madini mengine yanayoendelea kugunduliwa; Kutumia
fursa ya ongezeko la watu nchini kuleta manufaa ya kiuchumi (Demographic Dividend),
kwa kupunguza kiwango cha utegemezi, yaani uwiano kati ya watoto ambao ni tegemezi
na idadi ya watu wanaofanya kazi; na Kutumia fursa ya ongezeko kubwa la watu mijini
kwa kuifanya miji kuwa vituo endelevu vya ubunifu na ukuaji uchumi.
Maeneo
ya Kipaumbele kwa Mwaka 2014/15
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
masuala muhimu niliyoainisha, sasa naomba nielezee kwa kifupi maeneo ya kitaifa ya
kimkakati ya kipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2014/15. Maeneo
ya kipaumbele yanajumuisha miradi iliyoibuliwa katika progamu ya Matokeo Makubwa Sasa
ambayo yapo katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15,
kiambatisho A.
Maeneo ya Kitaifa ya Kimkakati na Programu
ya Matokeo Makubwa Sasa
Mheshimiwa Spika, kwa upande
wa Miundombinu, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni:
Nishati:
kuendelea kutekeleza miradi iliyoibuliwa chini ya programu ya Matokeo Makubwa Sasa
ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa bomba la Gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi
Dar es Salaam; na kuendelea kuboresha miundombinu ya ufuaji, usafirishaji na usambazaji
wa umeme mijini na vijijini. Aidha, Serikali itaendelea na uwekezaji katika vyanzo
vingine vya nishati mbadala, jadidifu na makaa ya mawe; na kuweka mazingira wezeshi
ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali za gesi asilia. Barabara: kutekeleza
miradi ya barabara iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan ujenzi
na ukarabati wa barabara zinazofungua maeneo yenye fursa za kiuchumi; na kuboresha
na kusimamia viwango vya usalama barabarani. Reli: Serikali itaendelea kuimarisha
reli ya kati hususan miradi iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwa
ni pamoja ukarabati wa miundombinu ya reli ikijumuisha majengo ya stesheni na madaraja;
kuanzisha mpango wa biashara (business plan) na mfumo wa madhubuti wa ufuatiliaji
wa mizigo; na ukarabati na ununuzi wa injini na mabehewa ya treni kwa ajili ya reli
ya kati. Maeneo mengine ni kuendelea kukamilisha upembuzi wa kina na kumpata mwekezaji
wa kujenga upya reli ya kati kwa kiwango cha geji ya kisasa; kufanya upembuzi yakinifu,
usanifu wa kina, na kutafuta wawekezaji katika miradi mipya ya reli; kuboresha usafiri
wa reli jijini Dar es Salaam na kuendelea kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi
wa reli. Bandari: kujenga na kuboresha miundombinu ya bandari iliyoanishwa kwenye
Programu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan kuboresha mfumo wa mawasiliano katika bandari
ya Dar es Salaam; na kuboresha miundombinu ya reli iliyopo bandarini. Aidha, Serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa bandari. Usafiri
wa Anga: kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi;
na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo ya kimkakati.
Maji Safi na Majitaka: kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika Progamu
ya Matokeo Makubwa Sasa hususan kuimarisha na kuongeza miundombinu ya maji vijijini
ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha
upatikanaji wa huduma za maji safi na majitaka katika Jiji la Dar-es Salaam na miji
mingine nchini kwa kuboresha, kukarabati na kuongeza miundombinu na vyanzo vipya. Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano: kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kuanzisha
maeneo maalum ya TEHAMA; utekelezaji wa mradi wa Anuani za Makazi na Misimbo ya Posta;
na kuhamasisha na kukuza tafiti za kimaendeleo.
Mheshimiwa
Spika, katika sekta ya Kilimo, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni:- kuendeleza miradi
ya kilimo katika programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwa ni pamoja na kuendeleza kilimo
cha kisasa kwenye skimu za wakulima wadogo wa mpunga; kutafuta mashamba kwa ajili
ya wawekezaji wakubwa; na kuanzisha mfumo wa maghala ya masoko ya mazao (collective
warehouse based marketing system). Maeneo mengine ni: utekelezaji wa miradi ya miwa
na mpunga katika maeneo ya mabonde ya Wami, Ruvu, Kagera, Kilombero na Malagarasi;
utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji katika ukanda wa SAGCOT; kujenga na kukarabati
miundombinu ya umwagiliaji, kuimarisha vituo vya tafiti za kilimo; kuwezesha na kuimarisha
Ushirika nchini; na kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Mifugo, maeneo yatakayopewa kipaumbele
ni: kuendeleza na kuboresha miundombinu ya mifugo kama vile malisho, majosho, na malambo;
kujenga na kuimarisha vituo vya uhamilishaji; kuongeza thamani ya mazao ya mifugo
na kuimarisha vituo vya tafiti za mifugo. Kwa upande wa sekta ya Uvuvi, maeneo ya
kipaumbele ni: kuimarisha usimamizi wa uvuvi katika eneo la Bahari Kuu ili kuongeza
mapato; kuimarisha zana za ukaguzi na uvunaji wa samaki; kukuza huduma na miundombinu
ya uzalishaji wa samaki na kuimarisha vituo vya tafiti za uvuvi.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Viwanda, maeneo ya kipaumbele ni: kuendelea
kutambua na kutenga maeneo ya ardhi ya uwekezaji, hususan katika Maeneo Maalum ya
Uwekezaji (EPZ/SEZ); ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini; kuongeza kasi
ya kuvutia wawekezaji na kujenga mazingira wezeshi katika sekta ya viwanda; kujenga
miundombinu muhimu katika kuendeleza mradi wa chuma - Liganga na mradi wa magadi soda
katika bonde la Engaruka; kuendeleza miradi ya kukuza ajira kwa vijana kwa kuimarisha
viwanda vidogo chini ya SIDO; kukuza maendeleo ya wajasiriamali wadogo na wa kati
kwa kuanzisha maeneo maalum ya viwanda na uhaulishaji wa teknolojia ya uzalishaji
wa matrekta na zana za kilimo.
Mheshimiwa Spika, katika
Maendeleo ya Rasilimali Watu, maeneo ya kipaumbele ni: kuendelea na utekelezaji wa
miradi ya elimu katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan mpango wa kuwezesha
wanafunzi na walimu kujifunza kwa shule za msingi na sekondari; kuimarisha mfumo wa
ruzuku ya kuendesha shule; na ujenzi wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
Maeneo mengine ni: kuendelea kutoa mafunzo katika nyanja maalum hususan katika gesi
na mafuta, chuma, urani, madini, umwagiliaji na maji; na kuendeleza elimu ya ufundi
stadi kwa kuongeza na kuboresha miundombinu na mitaala katika vyuo vya ufundi na vyuo
vya maendeleo ya jamii; upanuzi wa vyuo vya ualimu hasa katika masomo ya sayansi na
vituo vya utafiti; na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza
katika maendeleo ya rasilimali watu.
Mheshimiwa Spika,
katika sekta ya Huduma za Fedha na Utalii, maeneo ya kipaumbele ni: kuongeza mitaji
na matawi katika Benki ya Kilimo, Benki ya Rasilimali na Benki ya Wanawake; kujenga
uwezo wa utoaji huduma na mikopo; na mafunzo kwa wajasiriamali. Aidha, Serikali itaendelea
kupanga na kutangaza utalii; na kushirikisha sekta binafsi kuwekeza zaidi katika maeneo
yenye vivutio vya utalii.
Maeneo mengine
Muhimu kwa ukuaji wa Uchumi
Mheshimiwa Spika, pamoja
na kuwepo kwa maeneo ya Kitaifa ya kimkakati na Programu ya Matokeo Makubwa Sasa,
kutahitajika uwekezaji katika maeneo mengine ambayo yana uhusiano na maeneo ya kipaumbele
ya kitaifa. Miradi katika maeneo haya, itaibuliwa na sekta/mikoa na Mamlaka za Serikali
za Mitaa na sekta binafsi na kutekelezwa katika ngazi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, maeneo yatakayozingatiwa ni: Elimu/Mafunzo ya Ufundi,
Madini, Mifugo na Uvuvi, Misitu na Wanyamapoli, Afya na Ustawi wa Jamii, na Ardhi
Nyumba na Makazi. Maeneo mengine ni Usafiri wa Anga, Hali ya Hewa, Biashara na Masoko,
Utawala Bora, Ushirikiano wa Kikanda, Utambulisho wa Taifa, Sensa ya Watu na Makazi,
Katiba Mpya, Ajira na Mazingira.
Mheshimiwa Spika,
maelezo ya kina kuhusu maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2014/15 yapo katika Kitabu cha
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/15 (Sura ya tatu).
UGHARAMIAJI
WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2014/15
Mheshimiwa Spika, Makadirio
ya mahitaji ya rasilimali fedha ya kugharamia bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/15
ni shilingi bilioni 19,909.7. Kati ya hizo, shilingi bilioni 11,713.6 zitatokana na
mapato ya ndani, shilingi bilioni 1,148.0 ni mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara,
shilingi bilioni 2,898.2 ni mikopo ya ndani na shilingi bilioni 3,772.0 ni misaada
na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo. Kiasi hicho cha fedha kitagharamia matumizi
ya kawaida ya shilingi bilioni 14,642.4 na miradi ya maendeleo kiasi cha shilingi
bilioni 5,267.3 sawa na asilimia 26.45 ya bajeti ya Serikali. Kati ya bajeti ya
maendeleo, fedha za ndani ni kiasi cha shilingi bilioni 2,643.3 na kiasi cha shilingi
bilioni 2,624.0 ni fedha za nje.
Mheshimiwa Spika,
izingatiwe kwamba, kiwango cha bajeti ya maendeleo hakikujumuisha fedha kwa ajili
ya mfuko wa barabara na maendeleo ya rasilimali watu ambazo kwa mfumo wa sasa wa bajeti
zinapangwa kama sehemu ya matumizi ya kawaida japokuwa kiuhalisia ni matumizi ya maendeleo.
Kama vipengele hivyo vikijimuishwa, bajeti ya maendeleo inafikia takriban asilimia
31 ya bajeti yote.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kujikita katika kuwezesha sekta binafsi kuchangia katika kufanikisha utekelezaji wa
miradi ya maendeleo. Kipaumbele itakuwa ni kutumia rasilimali chache kuchochea uwekezaji
wa sekta binafsi pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya kibiashara na uwekezaji
ili kuvutia uwekezaji katika maeneo ya kipaumbele na yenye kuleta matokeo makubwa.
Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta
binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan, miradi ya miundombinu.
MAJUKUMU
YA UTEKELEZAJI Mheshimiwa Spika, mara baada ya Mapendekezo haya
kuridhiwa na Bunge, Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala za Serikali zitatakiwa
kuandaa na kuwasilisha Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha miradi itakayotekelezwa
katika sekta zao kwa mwaka 2014/15 wiki ya nne ya Januari 2014. Tume ya Mipango itafanya
uchambuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na wizara za kisekta na miradi
itakayopitishwa itajumuishwa katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15
na kitabu cha Bajeti ya Maendeleo 2014/15 (Vol 4). Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zitatakiwa kuainisha miradi ya maendeleo na kuwasilisha mapendekezo ya miradi hiyo
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kujumuishwa katika
kitabu cha Bajeti ya Maendeleo (Vol 4).
HITIMISHO Mheshimiwa
Spika, naomba sasa Bunge lako Tukufu likae kama kamati ya Mipango na kujadili mapendekezo
niliyowasilisha, ili Serikali iweze kunufaika na ushauri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge.
Baada ya kupata maoni ya Wabunge, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 utaandaliwa
na kuwasilishwa rasmi Bungeni mwezi Juni, 2014. Serikali itazingatia maoni na ushauri
wa Kamati ya Mipango ya Bunge zima na kuyafanyia kazi ipasavyo.