2013-10-30 09:05:08

Maendeleo ya kiuchumi yatoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu!


Askofu mkuu Justin Welby wa Kanisa kuu la Cantebury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Kiangalikani duniani anasema kwamba, mfumo bora wa uchumi na biashara hauna budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Askofu mkuu Welby ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza na wawakilishi kutoka katika sekta ya uchumi na biashara nchini Uingereza.

Anasema, mikakati ya uchumi na maendeleo haina budi kuwa ni sehemu ya mchakato unaopania kuhudumia mafao ya wengi ndani ya Jamii. Wachumi na wafanyabiashara wanapaswa kutekeleza nyajibu zao ndani ya Jamii kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili na utu wema; utu na heshima ya mwanadamu vikipewa msukumo wa pekee, jambo ambalo ni kinyume kabisa na mwelekeo wa wachumi na wafanyabiashara wengi wanaotafuta faida kubwa hata kwa gharama na mateso ya wananchi wengi.

Ulimwengu unaendelea kushuhudia mashindano ya utajiri wa mali na vitu, lakini ni watu wachache sana wanaothubutu kuwaonjesha jirani zao rasilimali na utajiri waliopewa kama zawadi na Mwenyezi Mungu. Viongozi wengi wa kijamii wanamwelekeo wa kutaka kujilimbikizia mali na utajiri kwa ajili ya mafao yao binafsi, bila kuzingatia kanuni ya mshikamano na utu wa mwanadamu.

Changamoto kama hii pia imetolewa na Askofu mkuu Vincent Gerard Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, aliyewachangamotisha wachumi na wafanyabiashara kutoa msukumo wa pekee katika kanuni ya mshikamano unaopania kumletea mwanadamu maendeleo endelevu katika masuala ya uchumi na biashara.

Mshikamano wa dhati ni kielelezo cha uwajibikaji unaotekelezwa ndani ya Jamii na kama sehemu ya mchakato wa uzalishaji wa utajiri kwa njia ya uwajibikaji mpana. Jamii inayosimikwa katika tunu hizi msingi anasema Askofu mkuu Welby inakuza na kupanua mwelekeo wa uchumi na biashara na kwamba, mwanadamu ataheshimiwa. Changamoto hizi zimeendelea kutolewa na Askofu mkuu Welby katika masuala ya biashara, uchumi na maendeleo kwa kuzingatia: sheria, kanuni na maadili mema.

Mchakato huu uwawezeshe wafanyabiashara wenye uwezo kusaidia juhudi za wafanyabiashara wadogo kutaka kujikwamua kutoka katika athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Familia zinaweza kujiunga na kuunda vyama vya ushirika kama mbinu ya kupambana na myumbo wa uchumi kimataifa unaoendelea kusababisha majanga makubwa kwa familia sehemu mbali mbali za dunia. Wafanyabiashara wanaweza kuwasaidia kwa njia ya mikopo yenye riba ndogo, wakisukumwa zaidi na kanuni ya auni, mshikamano na upendo. Sera na Mikakati ya kiuchumi haina budi kuwalenga wanyonge zaidi katika Jamii, ili nao waweze kuchangia katika ustawi na maendeleo yao.

Askofu mkuu Welby anakiri kuwa, hakuna majibu ya mkato katika kutafuta suluhu ya mikopo inayotolewa na Mabenki, lakini mikakati hii inapaswa kuongozwa na kanuni kwamba, shughuli za uchumi na biashara hazina budi kuelekezwa kwa ajili ya kuhudumia Jamii na wala si kwa ajili ya kuwakandamiza na kuwanyonya watu kutokana na umaskini wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.