FAO inapania kuboresha ufugaji ili uwe wa tija na mafao kwa Jamii husika!
Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja
wa Mataifa, FAO anasema, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono sera
makini za wafugaji na wakulima vijijini, ili kupambana na ukame wa kutisha katika
nchi za Sahel. Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuzuia ukame wala mafuriko, lakini inaweza
kuwasaidia wakulima wafugaji kupambana na baa la njaa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Wadau mbali mbali wako Kaskazini mwa Afrika ili kuangalia mikakati ya kilimo
cha umwagiliaji kama njia ya kupambana na baa la njaa katika maeneo ya Sahel. Ukame
wa kutisha umekuwa ni sababu ya kupanda kwa bei ya mazao ya chakula katika kipindi
cha miaka ya hivi karibuni na hivyo kupelekea hali ya wasi wasi wa uhakika wa usalama
wa chakula hasa miongoni mwa Jamii ya wafugaji, inayokadiriwa kuwa na watu millioni
16.
Hili ni kundi ambalo linahama hama kutafuta malisho na maji kwa ajili ya
mifugo yake, lakini limekuwa ikipambana na ukame pamoja na mafuriko; mambo ambayo
pia yameendelea kuchangia migogoro kati ya Jamii za wakulima na wafugaji Ukanda wa
Sahel. FAO inataka kuwasaidia wafugaji ili waweze kuanza ufugaji bora utakaowapatia
tija na kipato ili kuinua hali ya maisha ya familia zao.