Jumuiya ya uchumi Afrika Magharibi, ECOWAS katika mkutano wa viongozi wake wakuu,
imejadili na kupitisha maazimio yanayolenga kuboresha shughuli za kiuchumi sanjari
na usalama wa raia na mali zao. Viongozi hao katika mkutano wao uliofanyika mjini
Dakar, Senegal, wamepitisha kwa kauli moja kodi ya pamoja katika bidhaa zinazosafrishwa
katika nchi wanachama wa ECOWAS.
Kodi hii ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio
ya ECOWAS tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1975. Lengo ni kulinda biashara zinazozlishwa
na nchi wanachama wa ECOWAS. Viongozi hao pia wamekubaliana kuendeleza majadiliano
ya biashara kati ya ECOWAS na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pamoja na kufanya marekebisho
ya Itifaki iliyofikiwa mjini Cotonou, kunako mwaka 2000. ECOWAS inapania pamoja na
mambo mengine kuanzisha sarafu ya pamoja, ikiwezekana ifikapo mwaka 2015.
ECOWAS
kwa kushirikiana na wadau wengine, inapenda kuimarisha amani, utulivu na usalama kwa
kudhibiti biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya ambayo imekuwa ni chanzo cha
majanga kwa nchi nyingi za Kiafrika. Changamoto nyingine iliyojadiliwa na viongozi
hawa ni uharamia unaokwamisha mzunguko wa biashara Afrika Magharibi.