Watumiaji wa mitandao ya kijamii ni wadau wakuu katika utangazaji wa Injili! Millioni
10 si haba!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao
ya kijamii, amewashukuru wafuasi wake ambao hadi kufikia tarehe 26 Oktoba 2013 imefikia
watu millioni 10. Mtandao wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unaojulikana kwa anuani ya
@Pontifex umepata mafanikio makubwa katika ulimwengu wa watumiaji wa
mitandao ya kijamii.
Hii ni idadi ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia
wanaomfuata Khalifa wa Mtakatifu Petro katika ukurasa wake wa twitter unaosomeka kwa
lugha tisa kwa sasa. Hispania na Kiingereza kwa sasa ndizo lugha zinazoongoza kwa
kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao huu. Huu ni ujumbe wa maneno machache tu yanayogusa
moyo na akili ya mtu.
Alikuwa ni Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa Kumi
na sita, alipozindua mtandao huu wa kijamii na katika kipindi cha mwezi mmoja akawa
na wafuasi wapatao millioni moja. Ujumbe huu hutumwa pia na watumiaji wa mitandao
hii ya kijamii kwa marafiki, ndugu na jamaa zao, kiasi kwamba, idadi ni kubwa na inakaidiriwa
kwamba, watu wamefikia walau millioni 60, tofauti na wale wanaomfuata Baba Mtakatifu
moja kwa moja katika mtandao wake.
Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii,
limepokea ujumbe wa idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa moyo wa shukrani
na matumaini makubwa. Monsinyo paul Tighe anapenda kutumia fursa hii kuwashuruku watumiaji
wa mitandao ya kijamii wanaoendelea kumuunga mkono Khalifa wa Mtakatifu Petro katika
kueneza Ujumbe wa Imani, Matumaini na Mapendo miongoni mwa Jamii ya Kimataifa.
Watumiaji
hawa wa mitandao ya kijamii wamekuwa ni wadau wakuu katika Uenezaji wa Injili, dhamana
kubwa aliyokabidhiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa njia ya mitandao ya kijamii,
Baba Mtakatifu Francsiko kama alivyokuwa pia mtangulizi wake Papa mstaafu Benedikto
XVI anajitahidi kuhakikisha kwamba, kila wakati anawalisha watu kwa Habari Njema ya
Wokovu, licha ya tofauti ya imani na misimamo ya kijamii.