2013-10-29 14:13:25

Ukiukwaji wa misingi ya maadili na utu wema inaweza kuitumbukiza Tanzania katika majanga!


Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Monsinyo Aristaric Bahati, Paroko na Mwanasheria alipopewa Daraja Takatifu la Upadre. Jubilee ni kipindi cha neema na baraka, ni kipindi cha kuomba toba na msamaha, ili kuanza tena upya kwa ari na moyo mkuu zaidi pasi ya kukata tamaa kutokana na magumu yaliyopita.

Jubilee hii inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, unaotarajiwa kufungwa rasmi wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme wa ulimwengu.

Katika mahubiri yake, Askofu Msonganzila amesikitishwa sana na ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya viongozi wa umma pamoja na kukithiri kwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, wizi na watu kupenda mno utajiri wa haraka haraka unaopelekea baadhi ya wananchi wa Tanzania kujitumbukiza katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, ambayo yanaathari kubwa katika maisha na maendeleo ya watanzania.

Matukio kama haya ni viashiria vya kutoweka kwa misingi bora ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa watanzania, sanjari na kumong'onyoka kwa tunu bora za kimaadili na utu wema.

Askofu Msonganzila anawaalika waamini na watanzania kwa ujumla wao kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Mwalimu Kambarage Nyerere awe ni mfano bora wa kuigwa na viongozi kwa kuchukia baa la umaskini miongoni mwa watanzania na hivyo kuibua mbinu mkakati wa kupambana na umaskini, ili kuwajengea vijana imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Vijana wengi wamejitumbukiza katika vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu kutokana na kukata tamaa ya maisha sanjari na kuporomoka kwa maadili na utu wema, mambo ambayo ikiwa kama Tanzania haitayaangalia kwa makini yanaweza kulitumbukiza taifa katika "majanga". Amani anasema Askofu Msonganzila ni jina jipya la maendeleo endelevu ya mwanadamu, kwani bila amani, watu wataishia kwenye mauaji ya kinyama na litania ya migogoro ya kisiasa.

Kila mtanzania ajitahidi kuwa ni mlinzi, mjenzi na mtetezi wa amani ambao ni urithi mkubwa kutoka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa Taifa la Tanzania ambaye daima alitafuta mafao ya wengi ndani ya Jamii.

Naye Monsinyo Aristaric Bahati ambaye kwa taaluma ni Mwanasheria, amesema umoja na mshikamano wa kitaifa utaendelea kudumishwa ikiwa kama Katiba itakayopatikana haitakuwa na mizengwe ya kulinda maslhai ya kundi fulani na hivyo kusababisha ubaguzi miongoni mwa watanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.