Imarisheni amani na haki msingi za binadamu kwa njia ya demokrasia shirikishi!
Askofu Telesphory Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro amemsifia na kumpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha, kusimamia na
kuongoza vizuri mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya nchini Tanzania, licha ya tofauti
zilizojitokeza katika mchakato mzima.
Pia Askofu Mkude amewataka wananchi badala
ya kukaa na kulalamika, lazima wajitokeze na kutoa maoni yao ili kuboresha mchakato
huo na kuiwezesha Tanzania kupata Katiba nzuri ambayo itaiongoza kwa miaka mingine
50 ijayo. Aidha, Askofu Mkude amemwelezea Rais Kikwete kama kiongozi wa mfano ambaye
anawajali wananchi wake na kushirikiana nao katika kujitafutia maendeleo.
Vile
vile, Askofu Mkude amemsifia Rais Kikwete kwa kuendelea kusimamia na kudumisha amani
nchini pamoja na changamoto kubwa na nyingi anazokabiliana nazo katika kutimiza wajibu
wake huo kama kiongozi. Akaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha kwamba, amani na
utulivu vinadumishwa kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, ni jambo la msingi kuzingatia
utawala wa sheria na haki msingi za binadamu.
Askofu Mkude ametoa pongezi
na sifa hizo, Jumapili, Oktoba 27, 2013 wakati alipotoa neno ya shukrani mwishoni
mwa sherehe za Jubilee ya miaka 100 za Parokia ya Lugoba, Jimbo Katoliki Morogoro.
Askofu
Mkude amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo kwenye Kanisa
la Msalaba Mtakatifu ambako pia kuna shule aliyosoma Rais Kikwete mwanzoni mwa miaka
ya 1960: “Umefanya mengi sana wakati wa kipindi cha uongozi lakini moja ya mambo hayo
makubwa ni kuanzisha, kusimamia na kuongoza mageuzi makubwa ya kutungwa kwa Katiba
mpya katika nchi yetu. Tunakupa heko sana kwa kusimamia jambo hili ambalo litatuwezesha
sote kupata Katiba inayotokana na ridhaa ya wananchi.”
Miongoni mwa viongozi
wa dini na kilei waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Askofu Anthony Banzi, Askofu
wa Jimbo katoliki la Tanga.
Kuhusu nafasi ya wananchi katika mchakato huo,
Askofu Mkude amesema: “Tuache kunung’unika. Tutoe mani ya kuboresha Katiba yetu. Si
viongozi wengi wanatoa nafasi kama hii duniani kwa wananchi wao kushiriki katika kujadili
Katiba yao wenyewe. Kama asingependa, Rais angeweza kubakia na Katiba ya sasa ambayo
ni nzuri.”
Kuhusu suala la amani nchini, Askofu Mkude amesema kuwa ni muhimu
kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Kikwete katika kuibakiza Tanzania kisiwa cha amani
katika eneo lililojaa mizozo na migogoro isiyoisha. Amesisitiza: “Lakini wako wenzetu
hapa nchini ambao pengine hawaelewi maana ya amani. Amani ni muhimu sana kwa mambo
mengine yote. Tuacha malumbano na mapambano. Sasa sisi tukivurugana hapa tutakimbilia
wapi? Tumezungukwa na vita kila upande, huko mashariki tuna bahari, sasa tutakwenda
wapi tukiivuruga nchi yetu?”
Ameongeza Askofu, “Mheshimiwa Rais, napenda pia
kukupongeza kwa kuwa karibu na wananchi na kushirikiana nao katika mikakati ya maendeleo.
Hata kabla hujawa Rais, ukiwa bado Mbunge uliwafanyia mambo mengi na makubwa watu
wako. Angalia ule mradi wa maji wa Chalinze, nani alikuwa anapata maji katika ukanda
wetu huu?”
Mbali na kusoma katika Shule ya Kati ya Lugoba kati ya mwaka 1962
na 1965 wakati huo ikiitwa St. John Bosco’s Lugoba Middle School iliyokuwa inamilikiwa
na Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amekuwa anachangia maendeleo ya shule na Parokia
ya Lugoba.
Hata kabla ya kuanza kwa sherehe za miaka 100, Rais Kikwete alizindua
rasmi zahanati ya Kanisa ambayo yeye mwenye alisaidia kuikarabati na pia aliweka jiwe
la msingi kwenye ujenzi wa Ukumbi ambao unajengwa na Parokia hiyo kwa gharama ya Sh.
milioni 200.
Parokia ya Lugoba ilianzishwa miaka 100 na mapadre Cornel na Herman
kwa kushirikiana na wenyeji akiwemo Mtawala wa eneo hilo wakati huo, Mzee Kinogile.