2013-10-28 08:12:44

Wakuu wa Makanisa ya Mashariki kukutana na Papa Francisko mjini Vatican ili kujadili hali tete huko Mashariki ya Kati!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki katika mkutano maalum utakaojadili pamoja na mambo mengine hali tete ya Syria, Iraq na Mashariki ya Kati. Mkutano huu utahudhuriwa pia na viongozi wakuu wa Makanisa kutoka Mashariki ya Kati. hayo yamebainishwa na Kardinali Leonard Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati alipokuwa anafungua Mwaka wa Masomo 2013- 2014 kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki hivi karibuni.

Mkutano huu umeandaliwa na Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki na unatarajiwa kufunguliwa hapo tarehe 19 na kuendelea hadi tarehe 22 Novemba. Kauli mbiu itakayoongoza mkutano huu ni miaka 50 ya Makanisa Katoliki Mashariki baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii itakuwa ni fursa kwa viongozi wa Makanisa kutoka Mashariki kupembua kwa kina na mapana kuhusu hali ya: haki, amani na utulivu huko Mashariki ya kati pamoja na kushirikiana katika sala, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia amani na utulivu wananchi wa Mashariki ya Kati.

Itakumbukwa kwamba, mkutano kama huu uliwahi kufanywa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kunako mwaka 2009. Baba Mtakatifu mstaafu alitumia fursa hii kuwashuruku waamini wa Makanisa ya Mashariki kwa moyo wao wa ushirikiano, mshikamano na urafiki na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ndiyo tema itakayoongoza pia Maadhimisho ya Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ambao pia utajadili kuhusu Liturujia na Majiundo makini ya Familia ya Mungu, Mashariki ya Kati, lakini mkazo wa pekee ni kwa Makleri na Watawa.

Majiundo haya yanapaswa kujikita katika: masomo, maisha ya kiroho na kijumuiya pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji. Baraza pia linapania kufanya maboresho katika mitaala ya masomo kwa wanafunzi kutoka Makanisa ya Mashariki wanaosoma sehemu mbali mbali za dunia, jambo ambalo linapewa kipaumbele cha kwanza na Baraza lake anasema Kardinali Sandri anayewataka wanafunzi kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa, daima wakionesha utii kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.