2013-10-28 09:27:19

Ukosefu wa utawala bora, mafao ya wengi na athari za demokrasia ya mpito Barani Afrika ni chanzo cha maafa ya watu wengi


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linasema kwamba, ukosefu wa haki msingi za binadamu, maafa na hamu ya watu kutaka kupata hali bora ya maisha ni kati ya mambo ambayo yameendelea kuwasukuma watu kuhama katika nchi zao ili kupata nafuu ya maisha Ughaibuni na matokeo yake, watu wengi wanaendelea kufa maji hata kabla hawafikia nchi za ahadi kama ilivyojitokeza hivi karibuni kwenye Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia, ambako watu zaidi ya 360 walikufa maji!

SECAM inasikitika kusema kwamba, kuna idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi kutoka katika nchi za Pembe ya Afrika wanakimbia nchi zao kwa ajili ya kutafuta uhuru zaidi kutokana na hali ngumu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii wanayokabiliana nayo katika maeneo haya. Idadi kubwa ya wahamiaji hawa ni wale wanaotoka Somalia na Eritrea, nchi ambazo kwa miaka kadhaa zinakabiliwa na machafuko ya kisiasa, kivita na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Al Shabaab.

Hali ngumu ya maisha ni mambo yanayowasukuma baadhi ya wananchi kukata tamaa na hatimaye, kufanya maamuzi magumu yanayohatarisha hata maisha yao wenyewe. Hawa ni watu wanaotafuta maana ya maisha. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni SECAM iliandika Waraka wa Kichungaji kuhusu: Utawala bora, Mafao ya wengi na Demokrasia ya Mpito Barani Afrika. Katika waraka huu, Maaskofu wanasema kwamba, ongezeko la idadi ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika ni kiashilia kwamba, mambo si shwari kabisa. Watu wanatafuta fursa za ajira, elimu bora na huduma makini za afya, mambo ambayo yanaweza kufanyika hata Barani Afrika.

SECAM inasema kwamba, hata baada ya kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Bendera kwa nchi nyingi za Kiafrika, lakini bado machafuko ya kisiasa, vita, umaskini na ujinga vinaendelea kuhatarisha maisha ya watu wengi, kama ilivyotokea Kisiwani Lampedusa. SECAM kwa mara nyingine tena inauomba Umoja wa Afrika na Taasisi zake kuwa na mikakati makini ya kupambana na tatizo la wahamiaji na wakimbizi kutoka Barani Afrika; kwa kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wao ili kupunguza kasi ya wananchi wengi kutoka Barani Afrika kuwa na kishawishi cha kutaka kukimbilia Ulaya kwa kudhani kwamba huko kuna nafuu ya maisha.

Bara la Ulaya linapaswa pia kuwa na mikakati makini ya kuwasaidia wakimbizi wanaotafuta usalama na ubora wa maisha; wawapokee na kuwaonjesha wahamiaji na wageni moyo wa ukarimu!







All the contents on this site are copyrighted ©.