2013-10-28 11:12:20

Shule za Kanisa ni Jukwaa la majadiliano ya kidini, kiekumene na kijamii! Ni mahali pa kujenga fadhila na maadili mema!


Shule zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ni mahali muafaka pa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima; ni mahali ambapo elimu makini inatolewa ili kumwezesha mwanafunzi kupambana vyema na mazingira yake; ni mahali pa utamadunisho na jukwaa la majadiliano ya kidini, kiekumene na kijamii. Ndivyo alivyokazia Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake wa Kichungaji, Ecclesia in Afrika, Kanisa Barani Afrika.

Jimbo Katoliki Dodoma kwa miaka hamsini, limekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa njia ya Mashirika ya kitawa yanayofanya utume wake Jimboni humo! Hii ni elimu ambayo imekuwa ikitolewa kwa wote bila ubaguzi kwani mlengwa mkuu ni mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Africae Munus, Dhamana ya Afrika anakazia umuhimu kwa Kanisa kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwajengea watoto wa Afrika matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hii ni elimu ambayo inapaswa kujikita katika kweli za maisha.

Hivi karibuni, Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya huduma ya elimu inayotolewa na Shirika la Masista wa Misericordia wa Verona katika shule ya Sekondari ya Wasichana, Dodoma. Askofu Nyaisonga katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa huruma inayojikita katika mapendo kwa Mungu na jirani, kama kielelezo cha imani tendaji na kwa namna ya pekee wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.

Matunda ya upendo ni furaha, amani na huruma; upendo unadai ukarimu na kuonyana kindugu; upendo ni wema; hukuza hali ya kupokeana, hubaki huru bila kujitafutia faida; ni urafiki na umoja. Askofu Nyaisonga amekazia moyo wa huruma na mapendo kwa Mungu na jirani kama kielelezo cha ujenzi wa mshikamano wa upendo. Jina la shule hii ya Huruma liwe ni kikolezo cha matendo ya huruma yanayopaswa kutendeka ndani ya Jamii; yaani: kuwasaidia maskini, kuwatembelea wagonjwa na wafungwa magerezani pamoja na kuwazika wafu.

Upendo wa Kanisa kwa maskini na wanyonge ni mvuto wa Kiinjili na unawagusa maskini wa hali na mali. Kanisa linapowashughulikia maskini linawaonjesha tone la upendo na haki. Askofu Nyaisonga anaendelea kusema kwamba, Maandiko Matakatifu yanawachangamotisha Waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha huruma katika safari ya maisha yao hapa duniani, kwani huu ni utambulisho wa imani tendaji katika maisha ya Kikristo.

Askofu Gervas Nyaisonga anakazia kwamba: huruma, haki na upendo ni mambo yanayokwenda pamoja, lakini zaidi waamini wanapaswa kujenga na kukuza ndani mwao moyo wa kusamehe na kusahau, pasi na kulipiza kisasi kwani kisasi ni kazi ya Mungu. Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na wadau mbali mbali wa shule ya Sekondari ya Huruma, ambayo kwa kipindi cha miaka 50 imekuwa mstari wa mbele kusoma alama za nyakati kwa ajili ya kuwajengea wasichana uwezo wa kupambana na mazingira yao, hasa mkoani Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.