Ubinafsi ukizidi, familia inakosa mwelekeo wa furaha yake, Familia inayoishi imani
ni mwanga na chumvi ya dunia!
Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko
kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na
Familia za Kikristo. Kwanza kabisa, familia zinapaswa kuwa ni mahali pa sala, kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema, ukarimu na huruma yake katika maisha yao, daima
wakionesha moyo wa unyenyekevu, huku wakitambua udhaifu wao wa kibinadamu, na hivyo
kuhitaji kuonjeshwa upendo na huruma ya Mungu.
Huu ndio mwelekeo uliooneshwa
na mtoza ushuru anayepongezwa na Yesu katika Injili, kinyume kabisa cha Farisayo iliyejikuza
kupita kiasi. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko,
Jumapili tarehe 27 Oktoba 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia.
Baba
Mtakatifu anazichangamotisha familia za Kikristo kusali kwa unyenyekevu kwa kutambua
kwamba, wanahitaji kuonja uwepo wa Mungu kati yao. Familia zijifunze kusali sala za
kawaida, kutafakari Neno la Mungu kusali Rozari takatifu pamoja na kuombeana.
Familia
ni mahali pa kuhifadhia imani baada ya mapambano makali katika maisha kama alivyofanya
Mtakatifu Paulo, aliyejitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kushuhudia
imani kwa maisha yake, kiasi hata cha kuhatarisha uhai wake, akaguswa na kuchangamotishwa
na watu wa tamaduni mbali mbali, lakini akasimamama kidete kutangaza kweli za Kiinjili
bila woga! Hii ndiyo imani ambayo Mtakatifu Paulo aliyoipokea na kuirithisha kwa watu
wa mataifa, kiasi cha kupambana na kinzani nyingi.
Baba Mtakatifu anawaalika
waamini kuhakikisha kwamba, wanatunza imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia
ya ushuhuda wa maisha, ukarimu na mshikamano wa dhati. Familia za Kikristo zitambue
wajibu wake wa kimissionari katika uhalisia wa maisha yake ya kila siku, ili kweli
ziweze kuwa ni mwanga na chumvi ya dunia.
Baba Mtakatifu anazichangamotisha
Familia za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinafurahia imani, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi
Mungu ndiye chemchemi ya furaha na amani ya kweli; anasikiliza wanyonge wanapomkimbilia
kwa moyo wa unyenyekevu na kwamba, daima yuko karibu nao! Furaha ya kweli inapata
chimbuko lake si kwa vitu anavyomiliki mtu, bali kutoka katika undani wa moyo wa mtu
mwenyewe na uwepo wa Mungu katika maisha yake.
Hizi ni Familia zinazoonja
upendo wa Mungu unaowawajibisha kuwa wakarimu kwa jirani zao; uwepo wa Mungu unaowajengea
huruma na heshima kwa wote. Ubinafsi ukikithiri, familia itakosa mwelekeo na furaha
ya kweli itatoweka kama umande wa asubuhi. Lakini familia inayoishi furaha ya imani
ni mwanga na chumvi ya dunia, changamoto kwa familia kuiga mfano wa Familia Takatifu
ya Yesu, Maria na Yosefu. Mwishoni, Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewatakia
wote furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo!