2013-10-27 11:37:35

Sala ya Kanisa kwa mahitaji mbali mbali duniani!


Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakati wa Sala ya maombi, iliyotolewa kwa lugha mbali mbali, amewaombea watu wote duniani ili waweze kuwa na maisha bora, kila familia iweze kufurahia utulivu, uhakika wa fursa za ajira na makazi salama; maskini, wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii waweze kupata faraja na matumaini.

Kanisa limelisali na kuwaombea Wakristo wanaoteseka na kudhulumiwa; wafungwa na wote wanaonyanyaswa waweze kupata faraja; wateseaji na wadhulumati waweze kutubu na kuongoka; ili hatimaye, watu wote waweze kuwa na uhuru wa kidini.

Waamini wamesali na kuombea fadhila ya upendo; ili kwamba, wanandoa waweze kuishi kwa furaha kamili majitoleo na sadaka yao; watoto wakue na kuongezeka kimo na hekima; wazee na vikongwe waendelee kuwa na utulivu, kwa kutoa ushuhuda wa Kiinjili.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia, Waamini wamesali kwa ajili ya kuombea miito ya Kipadre na kitawa, ili shamba la Bwana liendelee kupata watendakazi; vijana na wasichana wajifunze sanaa ya kujitoa bila ya kujibakiza; na kamwe vijana wasiogope kufanya maamuzi magumu katika maisha yao na kwamba, wazazi wasiwe ni kikwazo cha watoto wao kujiweka wakfu kwa Kristo.

Ombi kwa lugha ya Kiswahili limetolewa na Tabita Janet Mhella kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa ajili ya kuombea Kanisa la Mungu, ili Kristo aweze kumjaza neema mchumba wake Kanisa; kila Mkristo aweze kukua katika utakatifu; Maaskofuna Mapadre waweze kumfuasa Yesu, Mchungaji Mwema; Watawa waweze daima kutoa harufu nzuri ya Kristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.