2013-10-27 14:18:30

Sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Familia


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia limekuwa ni tukio la imani kwani kabla ya Misa Takatifu, waamini wengi walipata nafasi ya kuungama ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho.

Mara baada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 27 Oktoba, 2013, Baba Mtakatifu Francisko amesali mbele ye Sanamu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, akiiendea kwa imani thabiti ili kutafakari umoja na upendo wa dhati, ili hatimaye, aweze kuzikabidhi Familia zote za Kikrito ambazo zinapaswa kuonja neema.

Familia Takatifu ni shule makini ya Neno la Mungu, Fadhila, hekima na nidhamu ya maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anaomba ili waamini waweze kuwa na jicho la kuona kazi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Familia Takatifu ni hifadhi aminifu ya Fumbo la Ukombozi.

Baba Mtakatifu anaomba fadhila ya ukimya, moyo wa sala katika familia ili ziweze kuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani; daima wanafamilia watamani utakatifu pamoja na kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha, kwa kusikilizana, kuelewana na kusameheana.

Familia Takatifu iwasaidie walimwengu kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha na kwamba, Familia ni hazina ambayo haina mbadala. Kila familia ijitahidi kupokea na kuenzi amani kwa ajili ya watoto na wazee; wagonjwa na wapweke; maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.