2013-10-27 09:16:16

Mwaka wa Imani: Kesha la Maadhimisho ya Siku ya Familia inayoishi imani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 26 Oktoba 2013 katika kesha la Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia, aliwaalika wanafamilia wote kushikamana kwa pamoja wakiwa na moyo na roho moja, kwani Kristo ndiye anayewategemeza.

Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulikuwa umesheheni umati wa watoto, vijana na wazee walioungana na Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, tukio ambalo limeongozwa na kauli mbiu "Familia inaishi furaha ya imani". Baba Mtakatifu anasema, amepata bahati ya kusikiliza kwa makini uzoefu, historia na mang'amuzi ambayo wameyasimulia wakati wa mkesha huo.

Ameguswa na magumu, umaskini, magonjwa na changamoto mbali mbali katika maisha ya kifamilia, lakini pamoja na mambo yote haya, bado waamini wanaalikwa kumwilisha furaha ya imani kwa Kristo anayewaalika kumwendea, ili aweze kuwapumzisha.

Hizi ni familia zinazoelemewa na mzigo wa ukosefu wa fursa za ajira, ukosefu wa upendo wa dhati, tabasamu la kukata na shoka pamoja na kushindwa kupokelewa. Hii ni mizigo ya ukimya unaozua wasi wasi na hofu ndani ya familia, kwani bila upendo wa dhati wanandoa watashindwa kuvumilia magumu yanayojitokeza katika sehemu za kazi. Baba Mtakatifu anawakumbuka wazee wanaoishi bila msaada; familia zinazoshindwa kuhimili kishindo cha makali ya maisha kutokana na sera tenge za uchumi; familia zinazokabiliana na magonjwa yanayohitaji huduma makini.
Familia zote hizi anasema Baba Mtakatifu zinakaribishwa na Yesu, ili zipate kupumzika kwani Yesu anazifahamu fika na kwamba, anataka kuzikirimia furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwake. Huu ndio ujumbe ambao Baba Mtakatifu anawaalika Wanafamilia kuukumbatia na kuusambaza kwa jirani zao. Wanandoa wanapaswa kuwa waaminifu katika taabu na raha, katika magonjwa na afya; wakipendana na kuheshimiana siku zote za maisha yao.

Hii ni hija ya matumaini kwa wanandoa, kwani hawatambui yale ambayo wanaweza kukumbana nayo katika safari ya maisha yao ya ndoa, lakini kama ilivyokuwa kwa Abraham wanamtumainia Mwenyezi Mungu bila woga huku wakiendelea kuwajibika mbele ya Mungu na Jamii inayowazunguka. Wanandoa wanapaswa kutekeleza utume wao wa kuunda familia na kwamba, neema inayotolewa na Sakramenti za Kanisa si kwa ajili ya kupamba ndoa, bali ni kwa ajili ya kuwaimarisha na kuwajalia ushujaa ili kusonga mbele na kusali kwa pamoja kama Jumuiya katika safari inayodumu maisha yao yote hadi pale kifo kitakapowatenganisha.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, wanandoa wanahitaji uwepo wa Yesu katika hija ya maisha yao, ili waweze kuwa na imani, wapokeane, wathaminiane na kuheshimiana kwa kutambua kwamba, wao si wakamilifu. Samahani, Naomba radhi na Asante ni maneno msingi katika kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati ndani ya familia. Wanandoa wajifunze kusamehana kila siku ya maisha yao.

Wajifunze kusali, kula na kupumzika kwa pamoja. Watekeleze matendo ya huruma kwa kuwatembelea wagonjwa na wazee. Pale ambapo hakuna upendo, furaha na sherehe vinatoweka kama ndoto ya mchana. Yesu ni Sakramenti ya furaha kwa njia ya Neno na Mkate wa uzima anaowakarimia wafuasi wake, ili waweze kuwa na furaha timilifu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanafamilia kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iliyoonesha utii kwa sheria, wakaenda Hekaluni na kupokelewa na Mzee Simeoni na Anna, waliobahatika kumwona Masiha aliyekuwa anasubiriwa na watu wengi. Wazee hawa wawili ni kielelezo cha imani kama kumbu kumbu, mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuwasilikiza na kuwaheshimu wazee kwani wote wanategemeana.

Baba Mtakatifu anasema, Familia takatifu ilitakatifuzwa kwa uwepo wa Yesu, hivyo wanafamilia hawana budi kushikamana na kutembea pamoja na Yesu, huku wakitolea ushuhuda wa imani yao na kwamba, Yesu anayo maneno ya uzima. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwatakia wanafamilia wote jioni njema.







All the contents on this site are copyrighted ©.