Familia zina wajibu wa kufanya kazi, kutoa malezi na makuzi bora pamoja na kusali!
Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume
ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, katika mahojiano na Radio
Vatican anasema kwamba, mwanadamu amepewa dhamana ya kushiriki katika mchakato wa
kuendeleza maboresho katika kazi ya uumbaji.
Hii ni changamoto
ya kutumia vyema vipaji, karama na nguvu alizo nazo kwa ajili ya kushiriki kikamilifu
katika kazi ya uumbaji kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo. Anakazia umuhimu wa elimu
na malezi bora yanayotambua uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele
vya mwanadamu na kwamba, utu na heshima ya kila mwanadamu vinapaswa kupewa kipaumbele
cha kwanza vinginevyo wanyonge watateseka na kudhulumiwa.
Ni vyema ikiwa kama
Jamii itawajengea wanafamilia uwezo wa kufanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa;
kwa kupata ujira halali na unaokidhi mahitaji msingi ya familia na kwamba, familia
zishiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya Jamii husika, ili kweli dunia
iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Familia zipate nafasi ya kupumzika
na kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu. Ikumbukwe kwamba, Jumapili ni Siku ya
Mungu, ni Siku ya Kristo ni Siku ya Binadamu, ni Siku ya Kanisa, ni Siku ya Mambo
ya Nyakati, hapa mwanadamu anapata fursa ya kutafakari maisha ya uzima wa milele,
akitambua kwamba, hapa duniani ni mpita njia, wala hana makazi ya kudumu.
Jumapili
ni siku maalum inayoziwezesha familia: kusikiliza Neno la Mungu na kushiriki Fumbo
la Ekaristi Takatifu, tayari kujitosa kimaso maso kueneza ushuhuda wa upendo unaobubujika
kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.