2013-10-26 13:31:59

Kitabu cha Yesu wa Nazareti ni hazina kubwa kwa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko amempongeza mtangulizi wake Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa zawadi kubwa kwa Kanisa kwa kuandika na kuchapisha Kitabu cha Yesu wa Nazareti. Ni vitabu ambavyo vimewaacha watu wengi wakiwa wameshikwa na bumbuwazi kutokana na sadaka na majitoleo yaliyooneshwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Licha ya kazi na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alipata pia fursa ya kufanya tafakari ya kina na hatimaye kuandika vitabu ambavyo ni hazina kubwa kwa Mama Kanisa. Haya ni matunda ya mwanataalimungu makini, aliyeandika si kwa mikogo ya kisomi, bali kama zawadi na hazina kwa Kanisa na Watu wote wenye mapenzi mema. Huu ni utajiri mkubwa wa Papa Benedikto wa kumi na sita, unaobubujika kutokana na tafakari, sala na upembuzi yakinifu katika taalimungu; kitabu ambacho kinaweza kusomwa na kueleweka na wengi.

Hii ni shukrani ya dhati kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na washindi wa Tuzo la Ratzinger kwa Mwaka 2013, Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013. Hazina hii ni kubwa na kwamba, haina kipimo, Mwenyezi Mungu ndiye peke yake anayeweza kutambua, kwani kwa njia ya kusoma na kutafakari vitabu hivi, watu wengi wamepata mwamko mpya wa imani: wameweza kuzama zaidi katika misingi ya imani na wengine wamepata nafasi ya kuweza kukutana na Yesu wa Nazaret kwa mara ya kwanza katika maisha yao, wakakirimiwa zawadi ya imani wanayoendelea kuitunza hadi sasa. Huu ni mchakato wa akili ya mwanadamu kuutafuta uso wa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, kazi kubwa iliyofanywa na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, imeamsha kipindi na ari mpya ya kutaka kujifunza Injili, Historia na Taalimungu kuhusu maisha ya Yesu. Huu ndio mwelekeo wa Kongamano la Tuzo la Joseph Ratzinger kwa Mwaka 2013. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wa wadau mbali mbali walioshiriki katika kufanyika Maadhimisho ya Kongamano hili.

Kwa namna ya pekee amewapongeza Professa Richard Burridge na Professa Christian Schaller washindi wa Tuzo la Ratzinger kwa Mwaka huu. Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya mtangulizi wake Papa Benedikto wa kumi na sita, amewatakia amani na furaha katika maisha na utume wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.