2013-10-26 08:47:06

Baada ya Miaka 10 ya maombi, Maaskofu Katoliki Zambia wapata kibali cha kuanzisha Kituo cha Televisheni! Si haba!


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia limeipongeza na kuishukuru Serikali ya Zambia kwa kutoa kibali kwa Baraza la Maaskofu katoliki Zambia kufungua na kuendesha kituo cha Televisheni kama sehemu ya mchakato wa utangazaji wa Injili kwa njia ya za mawasiliano ya kijamii.

Tangu mwaka 2002, Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia kwa mara ya kwanza liliomba kibali cha kuanzisha kituo cha Televisheni Kitaifa, lakini Serikali ikawa kimya kwa miaka yote hii, lakini Maaskofu waliendelea kuvuta subira hadi pale Serikali iliporidhia ombi lao hapo tarehe 18 Oktoba 2013.

Akizungumzia kuhusu tukio hili Paadre Paul Samasumo, Msemaji mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia anafafanua kwamba, wazo la kuanzisha Kituo cha Televisheni cha Kanisa ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa awamu ya kwanza ya Sinodi ya Afrika iliyofanyika kunako mwaka 1995 kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika njia za mawasiliano ya jamii kama vyombo muhimu vya Uinjilishaji Barani Afrika. Mkazo ukawekwa kwenye vituo vya radio na televisheni nchini Zambia.

Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linashiriki kwa hali na mali katika kurithisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili, Kiutu na Kitamaduni kwa watu wa nyakati hizi bila upendeleo kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili. Wazo hili ni changamoto iliyotolewa pia na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, aliyelichangamotisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linasoma alama za nyakati kwa kujikita katika Uinjilishaji wa vyombo vya mawasiliano ya jamii hata katika jukwaa hili jipya, linalohitaji pia kuonja "cheche za Injili".

Kituo hiki cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, kinalenga kuwahudumia wananchi wote wa Zambia bila ubaguzi, kwa kuzingatia: Maadili, Kanuni na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Maaskofu wanatambua changamoto kubwa zilizoko mbele yao katika kukiendesha, lakini ni muhimu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia: kiroho na kimwili. Ni kituo ambacho kinalenga Familia nzima.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia anasema Padre Paul Samasumo, litaendelea kugharimia vituo vya Radio vilivyoanzishwa na Majimbo kama vile Kituo cha radio Lutanda kilichoko Jimbo Katoliki la Chipata. Kituo cha Radio Sesheke kinatarajiwa kufunguliwa eneo la Sesheke na kwamba, Radio Maria Zambia sasa inaweza kusikika nchi nzima.

Hiki ni kituo ambacho kimeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya kiroho. Kwa hakika anasema Padre Paul Samasumo hii ni sauti ya Kikristo katika nyumba za wananchi wa Zambia, inayoleta mvuto na mguso wa kusikiliza!







All the contents on this site are copyrighted ©.