2013-10-25 07:28:17

Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, Dominika iliyopita tulipata kutafakari juu ya kudumu katika sala na sasa Dominika hii ya 30 ya mwaka C, tunatafakari nia ya sala yaani kwa ajili ya kukuza unyenyekevu na kwa ajili ya kuwaombea wengine. RealAudioMP3

Pamoja na kukua katika unyenyekevu bado kuna hatari zinazoweza kutokea katika maisha ya sala kama hatutakuwa waangalifu na kuweka mkazo na hasa tukijua sisi ni dhaifu na hivi tunahitaji msaada wa Mungu.

Mpendwa mwana wa Mungu, kusali kawaida si mara zote shughuli nyepesi na ya kujifariji. Mara kadhaa huleta hatari kama anayesali hajui maana ya sala yaani kukuza utukufu wa Mungu na kuwaombea wengine heri na fanaka. Sala yetu ni lazima iwe sala ambayo inazama katika mtima wa mioyo yetu ili kuweza kupata nguvu: kwanza ya kuweza kuendelea kusali na pia kujenga uhusiano wa mtoto na Baba yake na zaidi sana mapendo kwa wengine. Kuna wakati fulani mtu aweza kufikia hatua ya kusema sala haina maana, mbona mambo hayabadiliki, kumbe hakuna tofauti kati ya anayesali na asiyesali.

Lakini mpendwa msikilizaji kwa hakika kwa njia ya sala daima katika yule anayesali hutokea mabadiliko, walau basi yale ya kujitambua mwenyewe! Huwezi tena kujidanganya mwenyewe! Mwanga wa ukweli hujaa katika mtima wa moyo wako na hivi usukuma mtu kufikia hatua ya kusema ukweli na kukiri udhaifu wake mbele ya Mungu akisema “Bwana unihurumie kwa kuwa mimi ni mkosefu” Nani amefanya hilo ni yule Baba mtoza ushuru katika Injili, ni mfalme Daudi katika somo la kwanza.

Tukitafakari pia Barua ya kitume “Mwanga wa Imani” (Lumeni Fidei) tunaambiwa imani ya Kikristo ni mwanga mkamilifu ambao hutoka katika kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu. Ni mwanga ambao huleta mapendo na msamaha kwa wanadamu. Mwanga huu wa imani unajionesha tangu mwanzo wa uumbaji na bado unaendelea mpaka mwisho wa nyakati.

Imani huleta nguvu ya kuweza kuendelea kusali kwa unyenyekevu na hivi mpaka kufikia kuunganika na Kristu mzaliwa wa kwanza na kielelezo cha mfano wa unyenyekevu. Ni katika mwanga wa imani na kwa njia ya sala mmoja hugundua maana ya maisha na hujipatia faraja na hivi kuweza kuwa mtu wa kusukuma mbele taifa la Mungu.

Mara kadhaa kwa njia ya sala unagundua ukweli wa ndani ambao unakudai kubadilika na kuishi maisha ya kiinjili, hapa ndipo tuliowengi tunakumbana na shida na tunaona sala ni tatizo na hivi kujifariji tukisema tuachane nayo. Tunataka uhuru zaidi ambao kwa hakika si uhuru! Ndiyo kusema sala ni mwiba wa ukweli unaochochea mabadiliko kina, mabadiliko ya kiroho ili kumwelekea Mungu zaidi na zaidi.

Mpendwa msikilizaji, kuna njia nyingine ya kukwepa shida ya kusumbuliwa na ukweli! Ni kufanya sala aliyoifanya mfarisayo. Ni sala rahisi, yatosha kusema mimi nafanya hiki, mimi si kama yule, nasaidia mara nyingi kanisani!! Hapa sala inakuwa hatari tupu maana haiko katika kuutafuta ukweli bali kuufisha ukweli na kukumbatia upagani unaojikita katika mantiki ya kibinadamu, mantiki ya madaraka, mantiki ya kujipenda mtu mwenyewe na kupitiliza fudisho la Bwana.

Kama mmoja anazama katika ubinafsi huo tishio, basi huonesha upagani ambao si rahisi kuugundua lakini ulio wa kutisha katika historia ya mwanadamu, historia ya imani katoliki. Kwa hatua hii wapo waamini ambao namna yao ya kusali yaweza kuwa hatari na zaidi ni kinyume na ushuhuda wa mapendo kwa jirani, yafaa kukemewa na zaidi wakaelekezwa nini maana ya sala.

Mpendwa msikilizaji nasema hivyo kwa sababu bila kujua pengine sala huishia katika kujiabudu na kujitukuza wao wenyewe! Kumbe tuwe waangalifu katika maisha yetu, badala ya kusema mimi si tapeli, tuseme Bwana utuhurumie. Maana mmoja aweza kutokuwa tapeli lakini ugomvi kila siku nyumbani na mkewe au na mmewe!! Mmoja anasema mimi si mwizi, lakini pengine ni kwa sababu wizi wake ni wa kisomi zaidi!!

Mpendwa sala yetu iwe kama yamtoza ushuru, hatafuti kujitetea mbele ya Mungu bali anakubali shida yake na kisha anaisema mbele ya Bwana wake kwa upole na unyenyekevu. Mimi ni mdhambi! Kwa lugha ya Kigriki anaposema mimi ni mdhambi anatra kusema ule uhalisia wa kuwa mdhambi hasa!! Si rejareja! Hayuko katika kuhukumu wengine bali kuufuata mwanga wa ukweli unaogusa moyo wake na ukimdai abadilishe maisha yake na kweli anabadilika, na kutubu na kuifuata njia ya Bwana.

Mpendwa mwana wa Mungu, ni lini tutaweza kusali kama ndugu yetu huyu mtoza ushuru? Swali hili linaulizwa likitaka kuashilia udhaifu fulani katika sala yetu, yaani kusali bila kuzama katika mtima wa moyo! Ndiyo kusema tunaalikwa kusali katika uhalisia wetu na kwa kina!

Basi kufikia hapo lazima tujiachie na kujisalimisha mikononi mwa Mungu ili atufunde kwa makali yake ya mapendo na hivi tutoke mchicha kwa ajili ya wenzetu na taifa zima la Mungu. Kwa namna hiyo tutaweza kusali tukisema Baba mwenye huruma utuhurumie na utusadie kukupenda na kupendana sisi kwa sisi.

Katika sala mmoja huchota nguvu ya kuweza hata kupenya mawingu kadiri ya somo la kwanza na mfano wa sala kwa wengine tunaupata kwa Mtakatifu Paulo anayemwomba Mungu asiwahesabie hatia wale wote wanaozuia kazi ya kimisionari. Basi, nasi tujiunge katia maisha ya sala inayounganisha taifa la Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.