Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Jumapili tarehe 27 Oktoba 2013 linaadhimisha
Siku ya Mapadre Marekani. Hii ni fursa maalum kwa waamini wa Parokia mbali mbali nchini
Marekani kuweza kuunganika pamoja na Mapadre wao kwa: Ibada, Sala, tafakari na Majadiliano
ya kina kuhusu maisha na utume wa Mapadre ndani ya Kanisa.
Miaka 10 iliyopita,
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani lilianzisha Siku ya Mapadre Kitaifa, kama njia
ya waamini kuonesha moyo wa shukrani kwa huduma za maisha ya kiroho na kijamii inayotolewa
na Mapadre katika maisha na utume wao nchini Marekani. Hii inatokana na ukweli kwamba,
maisha na utume wa Mapadre unaangaliwa na vyombo vingi vya upashanaji habari "kwa
jicho la makengeza".
Tukio hili ni muhimu sana hasa kwa wakati huu idadi ya
miito ya Kipadre inapoendelea kupungua siku hadi siku. Nchini Marekani kuna Parokia
19,000 na kati ya hizi ni Parokia 4,000 tu ndizo ambazo zimebahatika kuwa na Padri.
Kumbe, kuna baadhi ya Mapadre wanalazimika kuhudumia zaidi ya Parokia moja kutokana
na uhaba wa Mapadre.