2013-10-25 08:27:18

Askofu asiyesali na kulitafakari kwa kina Neno la Mungu, atamezwa na malimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2013 majira ya jioni amewaweka wakfu Maaskofu wakuu wawili watakaoshiriki katika utume wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Hawa ni Askofu mkuu Jean Marie Speich, Balozi wa Vatican nchini Ghana na Askofu mkuu Giampiero Gloder, Rais wa taasisi ya elimu ya Kanisa.

Yesu Kristo mwanzoni mwa utume wake, aliwachagua mitume kumi na wawili waliokuwa wamejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mwishoni, hata mitume waliwaweka wakfu wasaidizi wao ili kushiriki katika utume wa kutangaza Injili ya Kristo, Mapokeo ambayo bado yanaendelea hadi leo hii.

Askofu anapozungukwa na Makleri wake, Yesu Kristo, Kuhani mkuu yuko pamoja nao! Kristo kwa njia ya maisha na utume wa Askofu anaendelea kutangaza Injili ya Wokovu; anaendelea kuwatakatifuza waamini kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Kristo analijalia Kanisa lake waamini wapya wanaojenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni Kristo kwa njia ya unyenyekevu na hekima ya Askofu anawaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili waweze kufikia furaha ya uzima wa milele!

Baba Mtakatifu anasema, Maaskofu wapya waliowekwa wakfu wanaingizwa katika hurika wa Kiaskofu; wanapaswa kuheshimiwa kama wahudumu wa Kanisa na wagawaji wa mafumbo matakatifu na kwamba, wanatakiwa kutolea ushuhuda wa Injili na utume wa Roho Mtakatifu katika azma ya kutakatifuza. Ni viongozi wanaopaswa kusikilizwa na kuheshimiwa kwa ajili ya Kristo.

Baba Mtakatifu amewaambia Maaskofu wakuu Jean Marie e Giampiero kwamba, watafakari kwa kina kwamba, wamechaguliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya mambo yanayomhusu Mungu. Uamskofu ni kielelezo cha huduma na wala si heshima. Askofu anapaswa kuhudumia na wala si kutawala. Huduma kwa familia ya Mungu ipewe kipaumbele cha kwanza.

Maaskofu wanatumwa kutangaza Injili kwa wakati unaofaa na ule usiofaa! Wanapaswa kukemea na kuonya, kufundisha na kutia moyo, daima wakijitahidi kuadhimisha Mafumbo matakatifu kama njia ya kupata utimilifu wa utakatifu wa maisha. Askofu ajibidishe kulitafakari Neno la Mungu na kusali, vinginevyo anaweza kumezwa na malimwengu! Kama walinzi na wagawaji wa Mafumbo matakatifu na viongozi wa Familia ya Mungu, wanapaswa kuiga mfano wa Kristo mchungaji mwema, anayewafahamu Kondoo wake, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake, huu ndio upendo unaobubujika kutoka kwa Askofu.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wakuu wapya kuwapenda wale wote ambao Mwenyezi Mungu amewakabidhi katika utume wao. Kwanza kabisa Makleri kwani wao ndio wasaidizi na jirani zao wakuu. Maaskofu wajenge utamaduni wa kuwasikiliza Makleri na kuwasaidia. Waoneshe upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii pamoja na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hawana budi kuwa karibu na waamini wao!

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wakuu wapya kujenga na kuimarisha moyo wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kushikamana na Maaskofu wengine wote, tayari kuyasaidia Makanisa yanayohitaji. Maaskofu wachunge Kondoo wa Kristo mintarafu maongozi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa la Mungu. Wakeshe katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; kwa kutambua kwamba, wao ni: Waalimu, Makuhani na Wachungaji. wakumbuke kwamba, Roho Mtakatifu anawainua katika unyonge wao kama binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.