Tanzania na China kuendeleza ushirikiano wa biashara na utalii kwa safari za moja
kwa moja kutoka China
Kampuni ya Ndege ya Hainan ya China imekubali kufanya safari za ndege za moja kwa
moja kutoka China hadi Tanzania ili kukuza sekta ya biashara na utalii baina ya nchi
hizo mbili.
Ahadi hiyo imetolewa Alhamisi, Oktoba 24, 2013 na Mwenyekiti wa
Shirika la Ndege la Hainan (Hainan Airlines), Bw. Chen Feng baada ya kuombwa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika mazungumzo yao alimwomba akubali ndege za shirika
lake ziwe zinatua Tanzania. Ndege za shirika hilo zinafanya safari kati ya China na
Angola kupitia anga la Tanzania.
Waziri Mkuu ambaye yuko ziara ya kikazi nchini
hapa, moja ya eneo ambalo amekuwa anaziomba kampuni za ndege za China ni kufikiria
kufanya safari ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara pamoja
na utalii pamoja na kuja kuweza katika ujenzi wa hoteli za kitalii. Pia alisema kuna
Watanzania wengi ambao wanakuja China kuchukua bidhaa hapa China lakini wanalazimika
kuunganisha safari mara tatu hadi nne kabla hawajafika China jambo ambalo alisema
linawaongezea gharama mno.
Akijibu maombi hayo ya Waziri Mkuu, Bw. Chen alisema
kutokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili, maombi yake watayafanyia kazi
na mojawapo ni hilo la kufungua safari za moja kwa moja za ndege kutoka China kwenda
Tanzania.
Lakini alishauri kuwa ili njia hiyo iendelezwe ni lazima kuwepo na
utaratibu wa kuhakikisha njia hiyo inakuwa ya kudumu kwa kuwa na abiria wengi na ikiwezekana
Tanzania kiwe kitovu cha usafiri wa anga kwa abiria wanaotoka nchi jirani wanaokwenda
na kutoka China.
Alisema ili kuweza kuwa kitovu cha usafiri wa China, ni lazima
abiria kutoka nchi jirani wapate usafiri wa uhakika wa kuwafikisha katika uwanja
wa ndege wa Dar es Salaam ambako wataunganisha safari yao wakitokea katika nchi zao.
Alisema
dawa pekee ya kufanikisha hilo ni kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la taifa ambalo
litashirikiana na Hainan kuhakikisha safari hizo zinakuwa zenye tija na faida kwa
kuwafikisha abiria hao kwenye kitovu cha usafiri wa kuunganisha kwenda China.
Pia
alisema ili Dar es Salaam iwe kitovu cha usafiri wa anga ni lazima kuwe na uwanja
wa ndege mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa wenye kukidhi mahitaji ya kimataifa
(international standards). Alisema kampuni yake iko tayari kuja nchini kushiriki katika
kupanua uwanja wa ndege utakaotumiwa na shirika hilo ili uwe wa kisasa.
“Tuna
wataaalam waliobobea katika eneo hilo, maana sisi wenyewe tu tunamiliki viwanja vya
ndege vipatavyo 16, hivyo mkitushirikisha mtakuwa na uwanja ambao kila aina ya ndege
inaweza kutua,” alisema mwenyekiti huyo wa Hainan Airlines.
Bw. Chen pia alisema
suala la utalii ni la muhimu zaidi kwani anatambua kuwa Tanzania kuna vivutio vingi
kama fukwe za bahari, mbuga za wanyama na vingine vingi na akaongeza kuwa shirika
lake lina uzoefu wa biashara ya utalii kwani lina kampuni zinazofanya kazi ndani ya
China na Hong Kong. “Tunaweza kusaidia kuwaleta Wachina waje kutalii Tanzania,” alisema
Bw. Chen na kusisitiza kuwa wataangalia katika kuwekeza kwenye hoteli karibu na hifadhi
za taifa.
Hainan ni moja ya mashirika makubwa ya ndege duniani. Ina ndege 470
na imeajiri wafanyakazi wapatao 1,000. Shirika hilo pia lina hoteli 500 za kitalii
duniani na lina viwanja vya ndege vipatavyo 16 vikiwemo vitatu vya kimataifa.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu alimweleza mwenyekiti huyo kuwa Tanzania inafanya juhudi
za kujikomboa kiuchumi; lakini bado inahitaji msaada wa China hasa katika masuala
ya usafiri wa anga ili iweze kupiga hatua kutoka hapo ilipo.
Alisema Tanzania
kuna shirika la ndege lakini liko taabani licha ya kuwa lina njia nyingi na akatumia
muda huo kumwomba mwenyekiti huyo wa Hainan kufikiria pia namna ya kuweza kufufua
ATC ili iweze kufanya kazi pamoja na Hainan.
“Ndio maana tunawakaribisha nyinyi
Hainan ni shirika kubwa ambalo naamini linaweza kuisaidia Tanzania katika eneo hilo
la usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanya safari za moja
kwa moja hadi Tanzania; lakini pia na kuangalia namna ya kulifufua shirika la ndege
la Tanzania (ATC),” alisema Waziri Mkuu.
Alimwomba Bw. Chen aangalie uwezekano
kuja kujenga hoteli za kitalii karibu na viwanja vya ndege. “Iweje hoteli za utalii
katika nchi yetu zijengwe na wafanyabiashara wa nchi za magharibi tu wakati na nyinyi
mna uwezo wa kufanya vizuri zaidi hata kuliko wao? Alihoji.