2013-10-24 11:54:05

Tafuteni utakatifu wa maisha kwa kusimama kidete katika haki na matendo ya huruma!


Wakristo wote wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika hija ya utakatifu kwani huu ni wito na lengo la kila mwamini. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wamezaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, mwaliko wa kuendeleza ile neema ya Ubatizo waliyoipokea ndani mwao, kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu.

Mwanadamu amekombolewa kutoka katika dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, mwaliko kwa waamini kujitahidi kufanya hija ya maisha ya haki na utakatifu, kwa kuendelea kumwamini aliyewakomboa na kuwastahilisha maisha ya uzima wa milele.

Hii ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican siku ya Alhamisi, tarehe 24 Oktoba 2013. Waamini wanaalikwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo adili, kama kielelezo makini cha imani tendaji; matendo ambayo yanamwezesha mwamini kujitakatifuza.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini walikirimiwa neema ya utakaso, lakini neema hii inachafuliwa kutoka na udhaifu wa binadamu na uwepo wa dhambi, ndiyo maana waamini wanahimizwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, inayoponya madonda ya dhambi na kumwonesha mwamini njia iendayo katika utakatifu. Waamini katika maisha yao ya kila wajitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani; pamoja na kujikita katika matendo ya huruma.

Waamini wajitahidi kujipatanisha na Mungu kwa njia ya wongofu wa ndani. Huu ndio mwaliko unaotolewa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake, ili kushiriki katika mchakato wa kuleta mabadiliko ya maisha ya watu duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.