2013-10-24 08:42:56

Miaka 25 ya Utawa na Upadre si haba kwa Waklaresiani nchini Tanzania


Hivi karibuni Padre George Nedumattan, Padre Bernard John pamoja na Padre Baskar Alamal Raj kutoka Shirika la Waklaresiani wanaofanya utume wao Afrika Mashariki, hususan nchini Tanzania na Uganda, wameadhimisha Jubilee ya Miaka 25 ya Upadre na Miaka 25 ya Maisha ya Kitawa kwa Padre Baskar Raj. RealAudioMP3

Hawa ni mapadre ambao wamejitosa kutangaza Habari Njema ya Wokovu bila ya kujibakiza; wakawa tayari kusimamia mafao ya wengi, wema, ukweli, utu na heshima ya binadamu. Kwa maneno na maisha yao, wameendelea kutangaza Injili nchini India, Tanzania na Uganda.

Akitoa neno la shukrani kabla ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Ukumbi wa Kituo cha Familia Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma, Padre Francis John, Mratibu mkuu wa Shirika la Waklaresiani, Afrika Mashariki amesema kwamba, mapadre hao wametumia muda wao mwingi kwa ajili ya kulea miito ya kipadre pamoja na shughuli za kichungaji kwa Majimbo ya Musoma, Tanzania na Jinja, Uganda.

Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki Musoma, iliungana na Mapadre hawa kwa ajili ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, wakiendelea kuwaombea mapadre hao neema, baraka na afya njema, ili waweze kujitosa kimasomaso kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kipadre na kitawa.

Katika mahubiri yake, Padre Bernard John aliyewahi kuwa mkurugenzi wa kituo cha familia cha Makoko, Jimbo Katoliki Musoma aliwataka waamini kujibidisha kutenda mema kwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaojionesha kwa namna ya pekee kwa kuwahudumia wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kama Mapadre na watawa wa Shirika la Waklaresiani, wanatumwa kuwahudumia ndugu zake Kristo, sehemu mbali mbali za dunia.

Upadre na utawa ni wito wenye misalaba, neema na baraka. Katika maisha na utume wao kama Wamissionari, wamewahi kuvamiwa na majambazi huko Morogoro; waliwahi kutekwa nyara na kuibiwa wakiwa mpakani kati ya Tanzania na Kenya eneo la Namanga. Baadhi yao wamewahi kupinduka na gari, lakini wakanusurika. Katika majanga yote haya ya maisha, wameonja pia huruma, upendo na ulinzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Leo hii wanathubutu kusimama Altareni ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa Mungu, kwa viongozi wa Kanisa Afrika Mashariki na kwa Familia ya Mungu, mahali pale ambapo wamehudumia kwa moyo wao wote! Wameonja na kushiriki “majanga” ya maisha ya waamini katika Parokia mbali mbali wanazoendelea kuhudumia nchini Tanzania na Uganda.

Mapadre hawa wanawaalika waamini kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mwanga unaobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Kila Mkristo anapaswa kukiri, kuadhimisha, kuishi na kusali imani yake kwa njia ya matendo, ili wengi waweze kuguswa na kuvutwa kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo, ili hatimaye, waweze kupata uzima wa milele.

Wamissionari hawa wanaowamba waamini kuendelea kusali kwa ajili yao, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Wanasema, wao wataendelea kuwa ni wahudumu wa Neno la Mungu, waadhimishaji wa Mafumbo ya Kanisa na matendo ya huruma, ili Injili ya Kristo iweze kuenea na kujikita katika mioyo ya Familia ya Mungu Barani Afrika.

Jubilee ni kipindi cha shukrani na moyo wa toba, hasa kwa yale ambayo wameshindwa kufanya kwa kuelemewa na mapungufu yao ya kibinadamu. Wanawaalika waamini kuendelea kuwa na moyo mkuu na wenye fadhila, ukarimu, ili kuonesha utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Wamissionari hao wanasema kwamba, ushirikiano kati yao na waamini umewezesha kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, afya na shughuli za kichungaji Jimboni Musoma na Jinja, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina. Kama Shirika limeendelea kuona changamoto ya elimu na afya kwa wananchi wa Jimbo la Musoma na Tanzania katika ujumla wake.

Wataaendelea kuifanyia kazi changamoto hii kwa kujenga na kuboresha shule wanazomiliki na kuziendesha, ili kuweza kukidhi matarajio ya Kanisa katika sekta ya elimu na afya. Jubilee hii ilihudhuriwa na Mapadre wa CMF kutoka Jumuiya zake zilizoko Tanzania na Uganda.

Kutoka Jimbo Katoliki la Musoma ni
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.