2013-10-24 11:23:08

Mahubiri ya Papa Francisko yakusanywa kwenye kitabu kimoja!


Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, kimechapisha mkusanyiko wa mahubiri ya Baba Mtakatifu Francsiko aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican kuanzia tarehe 23 Machi hadi tarehe 6 Julai 2013.

Kitabu hiki pia kinapambwa na mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu wakati wa hija ya kichungaji nchini Brazil wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Kitabu hiki ni mfululizo wa mkusanyiko wa vitabu vya maneno ya Baba Mtakatifu Francisko vinavyogusia: ombi lake kwa waamini kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; anawahimiza waamini kutokubali kupokonywa matumaini yao; furaha ya Uinjilishaji na kile kinachozungumzia furaha ya kukaa pamoja na Yesu.

Vitabu hivi vina lugha rahisi na nyepesi inayogusa akili na mioyo ya watu. Ni mahubiri ambayo yamepambwa kwa misemo, tamathali za semi, picha na majadiliano kati ya Baba Mtakatifu na msikilizaji au msomaji wa kitabu hiki, yote haya ni mintarafu mwanga wa Injili. Kitabu hiki ni mwongozo makini wa maisha ya kiroho, unaopenya undani wa mtu na kugusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu katika unyeti wake.

Ni kitabu ambacho kimesheheni utajiri wa maisha ya Kikristo kwa kuanzia kabisa katika: msamaha unaopata chimbuko lake kutokana na mateso, kifo na ufufuko wa Kristo; huduma ya maisha ya Kipadre pamoja na unafiki kuhusu Fumbo la Maisha na Utume wa Kanisa. Kitabu hiki ni mwaliko kwa msomaji: kufanya tafakari ya kina ili aweze kujichotea utajiri wa mafundisho yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema.







All the contents on this site are copyrighted ©.