Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete katika utekelezaji wa rufuku ya silaha
za mahangamizi!
Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa,
hivi karibuni wakati alipokuwa anachangia hoja kuhusu upigaji rufuku wa silaha za
kinyuklia duniani, kwenye Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa anasema, umefika
wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, silaha za maangamizi zinapigwa
rufuku.
Anasema, hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeonesha ujasiri wa
pekee na wa kihistoria kwa kupitisha azimio kuhusu uteketezaji wa silaha za kemikali
nchini Syria. Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna baadhi ya mataifa
makubwa duniani yanakwamisha jitihada hizi za Umoja wa Mataifa katika kudhibiti na
kufutilia mbali utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za Kinyuklia. Ni jambo
la aibu kwa baadhi ya nchi kushutumu matumizi ya silaha za maangamizi, lakini kwa
Jumuiya ya Kimataifa inapojadili kuhusu silaha za Kinyuklia, wanafunga kauli!
Umefika
wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzungumza na kutenda kwa mshikamano ili kukomesha
utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za maangamizi duniani. Katika ulimwengu
huu ambao umegeuka kuwa kama kijiji, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuendelea kuenzi
utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya mamillioni ya watu duniani kutokana
na vita.
Kuna haja ya kufutilia mbali falsafa ya vita vinavyosababisha majanga
na badala yake kuanza mchakato wa kupembua mahitaji msingi ya binadamu, ili yaweze
kushughulikiwa ipasavyo!