2013-10-24 14:47:28

Jibidisheni kujenga madaraja yanayounganisha tamaduni na imani za watu!


Baba Mtakatifu Francisiko, Alhamisi, tarehe 24 Oktoba 2013 amekutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Kituo cha Kiyahudi Kimataifa cha kutetea haki msingi za binadamu cha Simon Wiesethal.

Baba Mtakatifu amewashukuru kwa heshima wanayotoa kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye daima yuko mstari wa mbele kupambana na kila aina ya ubaguzi, hali ya kutovumiliana pamoja na chuki, bila kusahau kumbu kumbu ya Shoah, ili kufahamiana zaidi kwa njia ya majiundo makini sanjari na huduma za kijamii. Kanisa linaendelea kulaani kila aina ya dhuluma dhidi ya Wayahudi.

Anasema, tatizo la kutovumiliana linapaswa kushughulikiwa kwa ukamilifu hasa katika maeneo ambayo baadhi ya waamini wanadhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani au kabila anamotoka; hapa mafao ya wengi ndani ya Jamii yako hatarini na kwamba, kila mtu anapaswa kujisikia kwamba, anahusika!

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu nyanyaso na dhuluma wanazokabiliana nazo Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, changamoto kwa watu wote kuunganisha nguvu zao ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa kukutana, kuheshimiana, kufahamiana pamoja na kuhurumiana. Ili kufanikisha ujenzi wa azma hii, kuna haja ya kuwekeza katika majiundo makini yanayojikita katika ushuhuda, umoja na mshikamano kwa vijana wa kizazi kipya, daima wakiwa wazi kwa ajili ya kuukumbatia ukweli.

Vijana warithishwe utajiri unaofumbatwa katika majadiliano kati ya Wayahudi na Wakristo, magumu na changamoto walizokumbana nazo pamoja na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Juhudi za makusudi hazina budi kufanywa ili kuwajengea vijana ari na mwamko wa kupenda kukutana na kufahamiana kwa kuwajibika zaidi.

Kutokana na mantiki hii, Baba Mtakatifu Francisko anasema, huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii inapata kipaumbele cha kwanza. Viongozi na wadau mbali mbali waendelee kuwarithisha vijana tunu msingi za maisha ili kubomoa kuta za utengano na kujenga madaraja kati ya tamaduni na Mapokeo ya Imani za watu, daima wakisonga mbele kwa imani, ujasiri na matumaini.









All the contents on this site are copyrighted ©.