Familia inapaswa kuwa ni sehemu ya sera na mikakati ya kisiasa, kijamii, kiuchumi
na kiroho ili iweze kutekeleza dhamana yake!
Kardinali George Pell, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Sydney, Australia, hapo tarehe
23 Oktoba 2013 amefungua rasmi mkutano wa Baraza la Kipapa la Familia kwa Ibada ya
Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Askofu mkuu Vincenzo
Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia alizungumzia kuhusu mwono, changamoto,
matarajio na mikakati ya Baraza lake kwa siku za usoni.
Anasema, Familia ina
hazina kubwa katika maendeleo na mwanadamu: kiroho na kimwili, lakini pia familia
zinakabiliwa na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake. Kuna mmong'onyoko
mkubwa wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, hali ambayo inachangia kusambaratisha
familia nyingi duniani. Ubinafsi na kilio cha haki msingi za binadamu zinazosigana
na utu wema ni kati ya changamoto kubwa kwa familia katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na tekenolojia.
Ni matumaini ya Baraza la Kipapa kwamba,
familia itaendelea kuwa ni kiini cha mikakati na sera makini za kisiasa, kijamii,
kiuchumi na kiroho. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kutangaza Injili ya familia,
kwani ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu. Wazazi walioachana na kuoa au
kuoana ni changamoto katika malezi na makuzi ya watoto.
Wajumbe pamoja na
mambo mengine wamekazia umuhimu wa familia za Kikristo kutoa ushuhuda makini katika
maisha na vipaumbele vyao, kwa kuungana na Kristo kwa njia ya tafakari ya Neno la
Mungu, maisha ya Kisakramenti, Sala na Matendo ya huruma. Baraza la Kipapa la Familia
litaendelea kuhimiza utekelezaji wa katiba ya Familia Kimataifa sanjari na kuangalia
haki zake za kijamii.