Amani ya kudumu ni jambo muhimu sana huko Mashariki ya Kati!
Ujumbe wa Vatican unauangalia kwa matumaini makubwa mchakato wa kuanza tena kwa mazungumzo
kati ya Israeli na Palestina kama njia ya kudumisha amani na usalama huko Mashariki
ya Kati. NI matumaini ya ujumbe huu kwamba, mkutano wa pili wa Jumuiya ya Kimataifa
kuhusu Syria, utasaidia upatikanaji wa amani ya kudumu nchini humo.
Hii inatokana
na ukweli kwamba, mtutu wa bunduki unaporindima, wanaoathirika na kulipa kwa gharama
ya maisha yao ni wananchi wa kawaida! Kumbe, kuna haja ya kuwa na suluhu la kisiasa
itakayorudisha amani, usalama na utulivu huko Mashariki ya Kati sanjari na kuwasaidia
wahamiaji na wakimbizi kwa hali na mali, kama sehemu ya mchakato unaopania kuwapatia
wananchi wa eneo hili maendeleo endelevu.
Ni maoni ya Askofu mkuu Francis
Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa alipokuwa anachangia
mada hivi karibuni mada kuhusu hali ya usalama huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu
Francisko ameendelea kukazia umuhimu wa usalama, amani na utulivu huko Mashariki ya
Kati. Viongozi wa pande zinazohusika na mgogoro wa kivita nchini Syria hawana budi
kuacha mapigano kama hatua muhimu itakayosaidia mchakato wa majadiliano yanayolenga
upatikanaji wa suluhu ya kudumu nchini humo, katika mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa
unaotarajiwa kufanyika mjini Geneva, mwezi Novemba, 2013.
Askofu mkuu Chullikatt
anasema kwamba, hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni nne
ambao hawana makazi na wengine millioni mbili wameyakimbia makazi yao kwa kuhofia
usalama wa mali na maisha yao. Hali hii tete inaweza kuhatarisha usalama na amani
huko Mashariki ya Kati. Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kutoa msaada
wa hali na mali kwa waathirika wa mgogoro wa kivita nchini Syria bila ubaguzi wa kikabila
wala kidini.
Anasema, inasikitisha kuona kwamba, kuna idadi kubwa ya Wakristo
wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi zao kutokana na madhulumu ya kidini, hali
ambayo inawalazimisha kuikimbia historia ya maisha yao kwa takribani miaka elfu mbili
iliyopita, historia ambayo imejikita katika maisha na tamaduni za watu huko Mashariki
ya Kati. Ni jambo lisilokubalika kuona kwamba, madhulumu ya kidini yanaendelea huko
Mashariki kiasi cha kutishia amani na usalama wa Wakristo, kama ilivyotokea nchini
Iraq.