Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na serikali yake wameombwa
na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi (VETA) nchini kuangalia upya na kwa haraka,
umuhimu wa kuifanya marekebisho Sheria ya Manunuzi nchini kwa sababu sheria hiyo katika
hali yake ya sasa inarudisha nyuma maendeleo ya VETA na taasisi nyingine nchini.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Eng. Zebadayo Moshi amemwambia Rais Kikwete, Jumamosi, Oktoba 19, 2013,
kuwa ni vigumu kwa VETA kulazimika kwenda makampuni ya Toyota ama Scania kila mara
kununua magari mapya kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi wao kwa sababu Sheria hiyo
inazuia taasisi za umma kununua na kutumia vifaa vilivyokwishatumika.
Mkurugenzi
huyo alikuwa akizungumza leo kwenye Sherehe ya Ufunguzi wa Kituo cha Mafunzo ya Ufundi
cha Wilaya ya Makete (MDVTC) cha VETA, mjini Iwawa, mji mkuu wa Wilaya ya Makete,
ambako Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi na ambaye amefungua rasmi Kituo hicho.
Amesema
Eng. Mosha: “Sheria hii ya manunuzi itaua kabisa shughuli za VETA na taasisi nyingine
za umma nchini. Sisi siku zote, tunafundisha kwa vitendo na hivyo tunapotaka kumfundisha
mwanafunzi gari ni lazima tuwe na gari ama jinsi injini ya gari inavyofanya kazi ni
lazima tuwe na injini. Lakini kwa sababu Sheria hii inatuzuia kununua vifaa vilivyotumika,
tunalazimika kwenda Toyota ama Scania kununua gari jipya ama injini ya gari mpya.
Hili litatufikisha mbali kweli?”
“Majuzi tumeanzisha mafunzo ya ndege na injini
za ndege zinavyofanyakazi na kwa sababu ya Sheria hii ni lazima twende Kampuni ya
Boeing ya Marekani kununua injini ya ndege hiyo,” amesema kuwa wananchi walioshiriki
sherehe hiyo wakiangua vicheko.
Rais Kikwete amemwambia Mkurugenzi
Mkuu huyo wa VETA: “Nimesikia. Tutazungumza na wahusika kuona nini kinaweza kufanyika.
Tulipata kujaribu kuifanyia marekebisho sheria hii lakini wakubwa wale wakakataa na
kuruhusu taasisi moja tu ya Serikali kuweza kununua vifaa vilivyokwishakutumika.”
Kituo
hicho cha Ufundi cha VETA cha Wilaya ya Makete ni cha kwanza cha aina yake kujengwa
nchini kwa sababu ni cha kwanza kujengwa kwa dhana ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM
mwaka 2013 ambayo iliahidi kuanza kujenga vyuo vya ufundi katika wilaya badala ya
mikoa.
Aidha, Kituo hicho ni cha kwanza cha aina yake nchini kwa kuwa kimejengwa
na wanafunzi na wakufunzi wa Chuo cha VETA Mpanda, Mkoa wa Katavi, jambo ambalo limeokoa
gharama za ujenzi kwa kiasi cha Sh. bilioni 1.45 pamoja na kwamba mchanga wa ujenzi
uliokuwa unachukuliwa kutoka Makambako, mji mwingine wa Mkoa wa Njombe kwa sababu
Makete hakuna mchanga unaofaa kwa ujenzi wa mithili ya chuo hicho.
Chuo hicho
ambacho ujenzi wake ulianza Aprili 27 mwaka huu kwenye eneo la Kituo hicho la ekari
124 tayari kina wanafunzi 37 wanaoshiriki mafunzo ya ufundi ya ushonaji na uashi wakiwa
ni miongoni mwa wanafunzi 145,511 ambao wanaendelea na mafunzo katika vyuo vya ufundi
pote nchini.
Akizungumza na wananchi baada ya kufungua Kituo hicho cha kisasa
na cha kuvutia, Rais Kikwete ameipongeza VETA kwa kujenga chuo hicho cha kwanza kwa
dhana mpya ya kufikisha elimu ya ufundi wilayani.
Rais Kikwete pia ameitaka
VETA kuendelea kutoa mafunzo kulingana na mahitaji ya eneo husika na kutumia raslimali
zinazopatikana katika eneo ambako chuo kipo na kwa Mkoa wa Njombe amesema kuwa anataraji
kuwa VETA itajiekeleza katika ufundi unaohusiana na mazao ya mbao na wa viazi mviringo.
“Uhodari wa watu wa Makete hauwezi kuendelea kuwa kupanga viazi ama mbao tayari kuzipeleka
sokoni Dar Es Salaam, Uhodari sasa uwe ni wa kuanzisha viwanda vya fenicha baada ya
vijana wenu kupata mafunzo katika Kituo hiki ama kutengeneza mapochopocho yanayotokana
na viazi. Tunahitaji siku moja na sisi kusema kuwa fenicha hii safi imetengenezwa
Makete.”
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa VEAT iangalie uwezekano wa kuwapatia
wahitimu wake zana na vifaa vya kuanzia kazi za kujitegemea baada ya kumaliza mafunzo
yao. “Lazima vijana hawa tuwasaidie kujiajiri kwa sababu tunahitaji sana mafundi stadi
na mafundi mchundo kuongeza thamani kwenye uchumi wetu.”
Rais Kikwete yuko
katika ziara ya siku saba kukagua na kuzindua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa
Njombe