Baraza la Kipapa la Familia kuanzia Alhamisi tarehe 24 Oktoba hadi tarehe 25 Oktoba
2013 linaendesha Kongamano la Kimataifa kuhusu haki ya familia, hasa wakati huu ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaposhuhudia athari za myumbo
wa uchumi kimataifa pamoja na kumong'onyoka wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Baraza la Kipapa la Familia wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, linapenda
kuchukua nafasi hii kuwashirikisha wadau mbali mbali katika kongamano linalopania
kuchambua kwa kina na mapana haki msingi za familia. Kongamano hili linakwenda sanjari
na mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Familia, utakaohitimishwa kwa kesha la Mwaka
wa Imani kwa ajili ya familia; tukio ambalo litazishirikisha familia kutoka sehemu
mbali mbali za dunia. Muda huu ni kipindi cha sala na tafakari ya kina kuhusu haki
msingi za familia katika ulimwengu mamboleo.
Licha ya viongozi wakuu kutoka
Baraza la Kipapa la familia kushiriki katika kongamano hili, kutoka Barani Afrika
ni Kardinali John Onaiyekani, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria. Kati ya
mambo yatakayojadiliwa ni Katiba ya Familia Kimataifa na mielekeo mipya ya haki msingi
za kifamilia.