Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano
na Radio Vatican anabainisha kwamba, Kanisa limeendelea kuwekeza katika taasisi ya
Familia kwa kutambua kwamba: Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, chemchemi ya imani,
matumaini na mapendo, changamoto endelevu ya kujenga na kuimarisha familia ili ziweze
kutekeleza wajibu wake barabara ndani ya Jamii na Kanisa.
Anasema, Kanisa
imara na thabiti linajengeka katika msingi wa familia bora inayoonesha upendo kati
ya Baba, Mama na Watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Familia
ni chemchemi ya miito mbali mbali ndani ya Kanisa kiasi kwamba, hata wito wa familia
yenyewe unapata chimbuko lake ndani ya familia. Familia zinapaswa kuimarishwa ili
kulifahamu Fumbo la Utatu Mtakatifu; kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, Kusali na kuwa
kweli ni kielelezo cha maadili na utu wema katika Jamii inayowazunguka.
Katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Familia zinachangamotishwa kuwashirikisha majirani
zao imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kama njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Familia
itambue kwamba, ni Kanisa dogo la nyumbani, nguzo thabiti ya malezi na makuzi ya:
imani, maadili na utu wema.
Padre Raymond Saba ambaye ameteuliwa hivi karibuni
na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Katibu mkuu mpya, kuchukua nafasi ya
Padre Anthony Makunde aliyemaliza muda wake wa uongozi, anawaalika wanafamilia kuhakikisha
kwamba, wanashirikishana imani yao kuanzia katika familia. Baba, Mama na Watoto wasaidiane
kusoma na kulitafakari Neno la Mungu kwa pamoja; wasali na kuonjeshana tone la upendo,
huruma na msamaha; familia kwa pamoja ijitahidi kushiriki katika maadhimisho mbali
mbali ya Sakramenti za Kanisa kwa njia ya ushiriki mkamilifu.
Padre Saba anasema,
ikiwa kama familia zitatekeleza wajibu huu msingi kwa hakika familia za Kikristo zitakuwa
ni shule ya sala, amani, upendo, mshikamano na uaminifu kama alivyokumbusha Mwenyeheri
Yohane Paulo wa pili alipotembelea nchini Tanzania.