Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, upendo na mshimamano wa dhati na Kristo
Yesu!
Bikira Maria mwenyeheri, kwa kipaji cha dhima na umama wa kimungu unaomwunganisha
na Mwanae Mkombozi, na kwa neema zake za huduma zake za pekee ameunganika kwa undani
na Kanisa. Mama wa Mungu ni kielelezo cha Kanisa, kwa habari ya imani, mapendo na
umoja kamili na Kristo, kama alivyowahi kufundisha Mtakatifu Ambrosi.
Ni maneno
ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 23 Oktoba kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuhusu dhamana na nafasi ya
Bikira Maria kama kielelezo na mfano wa Kanisa. Bikira Maria ni mfano na kielelezo
cha imani inayoonesha mpango wa Mungu katika maisha yake, kiasi cha kumchagua kati
ya wanawake wote kuwa ni Mama wa Mkombozi.
Ni mwanamke aliyejaa neema na ambaye
alikubali mpango wa ukombozi uliotekelezwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Ukubali
wa Maria ukamwezesha kuwa ni Mama wa Kristo, kielelezo cha hija ya imani iliyofanywa
na waamini mbali mbali waliokuwa wanasubiri wokovu katika maisha yao. Bikira Maria
ni kielelezo cha imani ya Kanisa katika Fumbo la Umwilisho, linaloonesha upendo wa
Mungu usiokuwa na kifani kwa binadamu.
Bikira Maria aliweza kumwilisha imani
yake katika uhalisia wa maisha ya kila siku, akajenga majadiliano ya kina kati yake
na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala iliyomwezesha kudiriki kusimama chini ya Msalaba.
Umama wake anasema Baba Mtakatifu unawakumbatia wanadamu wote katika Fumbo la Umwilisho.
Ni mwanamke aliyejikita katika tafakari ya kina, mwanafunzi amini wa Kristo, changamoto
kwa waamini kumwachia nafasi Bikira Maria ili aweze kuwaongoza katika imani kwa Kristo.
Bikira
Maria alikuwa ni mfano wa huduma ya upendo unaojionesha kwa kumtembelea na kumhudumia
binadamu yake Elizabeth aliyekuwa mjamzito. Ni Mama aliyeonesha ukarimu wa pekee kwa
kumbeba tumboni mwake Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu,
aliyewakirimia watu furaha ya kweli. Bikira Maria anataka kuwapatia watu wote zawadi
kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo ni Yesu Kristo.
Baba Mtakatifu anasema,
Yesu anawakirimia waja wake: furaha, amani na upendo. Kanisa linatumwa na Kristo kwenda
ulimwenguni kote ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kila mwamini
ni sehemu ya Kanisa, kumbe anao wajibu wa kuhakikisha kwamba, anampeka Yesu kwa watu
wa mataifa, kwa kuwashirikisha na kuwaonjesha wengine tone la upendo unaoponya na
kusamehe; upendo unaojitosa kimasomaso kwa ajili ya mafao ya wengi; upendo unaowaunganisha
watu chini ya mchungaji mmoja ambaye ni Kristo mwenyewe, kwa kusaidiana na kutaabikiana.
Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria ni kielelezo cha umoja mkamilifu na Yesu
Kristo kwa njia ya maisha na matendo yake. Bikira Maria alikuwa ni mwanamke wa sala
na kazi, kiasi hata cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba, hapo akajiunga na Mwanaye
mpendwa Yesu Kristo, katika sadaka safi, isiyo na waa wala makunyanzi kwa ajili ya
ukombozi wa binadamu. Akashiriki mateso ya Mwanaye kama njia ya kutekeleza mapenzi
ya Mungu katika maisha yake; utii unaoshinda dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa waamini
kuungana na Yesu katika maisha yao, kwa kudumisha urafiki wa dhati hata katika ile
Njia ya Msalaba.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusali Rozari
Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani pamoja na tunu msingi za maisha ya Kiinjili
kuweza tena kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi
mema. Amewapongeza waamini wote wanaoendelea kuadhimisha kwa ari na moyo mkuu Mwaka
wa Imani sehemu mbali mbali za dunia.
Mwishoni anasema, kila mwamini anachangamotishwa
na Mama Kanisa katika mwezi Oktoba kuwa ni mmissionari anayetumwa kutangaza Injili
hadi miisho ya dunia, kwa kuwashirikisha jirani zake, upendo wa Kristo.