2013-10-22 09:40:51

Ujumbe wa Maaskofu kutoka Makanisa ya Mashariki kwa Familia ya Mungu!


Maaskofu Katoliki kutoka Mashariki mwa Bara la Ulaya, hivi karibuni wamehitimisha mkutano wao wa Mwaka uliokuwa umedhaminiwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 1150 tangu walipowasili watakatifu Cyrili na Metodi miongoni mwa wananchi wa Slovakia. Imekuwa ni nafasi pia ya kuadhimisha Mwaka wa Imani kwa kusali kwa pamoja ile sala iliyotungwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kwa ajili ya wananchi wa Slovakia.

Maaskofu pamoja na mambo mengine wamejadili kwa kina na mapana dhana ya utamadunisho mintarafu mchango wa watakatifu Cyril na Metodi katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu sanjari na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa sasa katika ngazi ya Makanisa mahalia na Ulaya katika ujumla wake.

Maaskofu mara baada ya kuhitimisha mkutano wao wa Mwaka, wamewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema ujumbe wa: imani, matumaini na mapendo, kwa kutambua kwa dhati kabisa umuhimu wa ujumbe wa Habari Njema iliyotangazwa na watakatifu Cyril na Metodi. Maaskofu wanasema, utamaduni ambao unasigana kimsingi na misingi ya Injili hauwezi kamwe kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na tunu bora za maisha ya kifamilia yanayojengeka katika msingi wa haki, amani na utulivu.

Maaskofu wanasema, utamaduni unaomng'oa Mungu katika maisha ya watu, unamwongezea mwanadamu msongo wa mawazo, hali ya kukata tamaa na hatimaye, kifo. Kanisa kwa upande wake, linapenda kutangaza na kuenzi utamaduni wa maisha na maisha unaojikita katika udugu, upendo na mshikamano wa dhati kwa maskini, wahamiaji, wakimbizi na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha.

Huu ni utamaduni unaotambua na kuthamini uwepo wa Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu, kwa kutambua kwamba, Mungu anampenda mwanadamu na kwamba, Yesu Kristo amemwaga damu yake Msalabani ili aweze kumkirimia mwanadamu uzima wa milele.

Maaskofu wanasema kwamba, wanatambua fika matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wa Bara la Ulaya: hii ni pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; athari zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika janga la umaskini wa hali na kipato; vitendo vya kigaidi, vita, migogoro na kinzani za kijamii na kisiasa pamoja na ubaguzi wa rangi. Huu si myumbo wa uchumi peke yake, bali ni mmong'onyoko wa tunu msingi za maisha ya kiroho, changamoto kwa Wakristo kutolea ushuhuda wa tunu bora za maisha ya kiroho walizorithi kutoka kwa Mababa wao wa imani.

Maaskofu wanasema, wanataka kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa furaha na ari kubwa zaidi, kwani watu wana kiu ya uwepo wa Mungu anayetoa maana ya maisha na uwepo wao hapa duniani; waamini wakiwa daima wanasaidiana kubeba Msalaba, wakitambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao! Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele na changamoto kwa Wakristo na watu wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa ushirikiano na mshikamano katika mchakato unaopania kuimarisha utamaduni wa majadiliano unaojikita katika: ukweli, uhuru, haki, heshima na kuvumiliana.

Kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni mdau katika Uinjilishaji Mpya mintarafu mwaliko wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kutambua na kuthamini hazina ya Mapokeo ya Kanisa yanayopaswa kupyaishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa Barani Ulaya.

Maaskofu wanasema, katika mkutano wao, wamegusia pia hali na maateso ya watu sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee mateso ya wananchi wa Syria na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Maaskofu wanapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu mahalia na Wapenda amani kukazia kwa mara nyingine tena juhudi za majadiliano ya kina ili kupata suluhu ya kudumu katika maeneo haya kwa kukazia: misingi ya haki, amani pamoja na kuheshimiana hata katika tofauti zao za kidini na kiimani.

Maaskofu wanasema, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kupiga rufuku biashara ya silaha katika maeneo haya kwani hizi zimekuwa ni kichocheo kikuu cha migogoro na vita huko Mashariki ya Kati. Mwishoni, Maaskofu wanasema, kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu na ya watakatifu Cyril na Metodi, wanaombea amani na utulivu kwa wananchi wote wa Bara la Ulaya na ulimwengu katika ujumla wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.