2013-10-22 08:47:36

Tambueni juhudi na malengo ya Maaskofu katika sekta ya elimu ya juu Tanzania


Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, kilichoko Jijini Mwanza, Tanzania, hivi karibuni kilifungua rasmi mwaka wa masomo kwa kipindi cha mwaka 2013- 2014 kwa kuomba mapaji ya Roho Mtakatifu. Ibada hii ya Misa Takatifu iliongozwa na Mheshimiwa Dr. Respicius Rugemalira, Mwanasheria mkuu wa SAUT. (Corporate Counsel). RealAudioMP3

Katika mahubiri yake, Padre Rugemalira aliwakumbusha wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT kwamba, Roho Mtakatifu anafundisha, anaimarisha, anakumbusha, analinda na kuhuisha uumbaji. Roho Mtakatifu anaongoza moyo wa binadamu, anavuvia na kuendeleza ufunuo; anawaombea watu sanjari na kuwaongoza waamini katika kuutafuta na kuufahamu ukweli. Roho Mtakatifu anawaongoza waamini kwenye hija ya umoja kamili, anawakirimia wote mapaji yake saba.

Jumuiya ya Chuo Kikuu cha SAUT katika Ibada ya Misa ya Ufunguzi wa Mwaka wa Masomo, ilipania kumwomba Roho Mtakatifu awaangazie, awakumbushe na kuwaombea ili waweze kutekeleza mwono na utume wa Chuo Kikuu cha SAUT kadiri ya Malengo na Matakwa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Padre Rugemalira amesema kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maisha na utume wake, limeamua kuwekeza zaidi na zaidi katika elimu ya juu kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Maaskofu Katoliki wanapenda kuona kwamba, Vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania zinatoa ujuzi, maarifa na elimu ya hali ya juu kwa kuzingatia misingi ya maadili na utu wema; utambulisho wa kitaifa, ili hatimaye, waweze kuwa ni raia wanaowajibika katika ujenzi wa Jiji la Mungu hapa duniani kama alivyosema Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa.

Maaskofu wanapenda kuona kwamba, elimu inayotolewa nchini Tanzania katika ujumla wake inasaidia ujenzi na ukomavu wa mtu mzima anayepaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kutokana na changamoto hii iliyoko mbele yao, Chuo Kikuu cha SAUT kinapaswa kuwa ni mahali ambapo elimu inatolewa kwa ubora na viwango vya juu; mahali ambapo wanafunzi wanaweza kufanya tafiti pamoja na kutoa huduma kwa Jamii inayowazunguka.

Wanafunzi wajengewe uwezo wa kutafuta na kusimamia na kutetea ukweli, kwa kuzingatia uwazi, uaminifu na huduma ambayo kimsingi inapaswa kujikita katika weledi, umakini na majitoleo. Katika maisha yao kama wanafunzi, wanapaswa kujenga na kuimarisha moyo wa kijumuiya kwa kulinda na kuheshimu mali ya umma na ile ya mtu binafsi.

Chuo Kikuu cha SAUT anasema Dr. Respicius Rugemalira, kinapaswa kuwa ni mahali ambapo wanafunzi wanapata elimu bora na wala si bora elimu, ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha, daima wakiwa tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Watanzania wote; utu na heshima ya kila binadamu vikiwepa kipaumbele cha kwanza.

Anasema, Ibada hii ya Misa takatifu iwakumbushe wadau mbali mbali wa Chuo Kikuu cha SAUT kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, hekima na busara, kila mtu akijitahidi kutekeleza wajibu na dhamana yake kikamilifu. Roho Mtakatifu awaongoze kwenye umoja na ukweli mkamilifu, wanapotekeleza wajibu na dhamana waliyokabidhiwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania.

Kutoka Chuo Kikuu cha SAUT, Mwanza ni
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.