Mwenyezi Mungu anapenda kuponya madonda ya dhambi na mauti!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa
cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, siku ya jumanne, tarehe 22 Oktoba 2013
amekazia mambo makuu matatu: tafakari ya kina, ukaribu kwa Mwenyezi Mungu na utashi
wa kutaka kutekeleza mapenzi ya Mungu. Haya ni mambo muhimu sana yanayoweza kumsaidia
mwamini kulifahamu Fumbo la Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, haiwezekani kwa
mwamini kulifahamu Fumbo la Mungu kwa kutumia juhudi za akili yake kwani Mwenyezi
Mungu, mwingi wa huruma na mapendo amejichanganya katika maisha ya mwanadamu, ili
aweze kuwaponya madonda yao ya ndani, kama alivyofanya Yesu mwenyewe.
Fumbo
la Mungu ni jambo linaloendelea kumshangaza mwanadamu katika hija ya maisha yake ya
imani ndiyo maana Mtakatifu Paulo anajitaabisha kuwafafanulia waamini kuhusu Fumbo
la Ukombozi lililotekelezwa na Mungu, linaloweza kufahamika kwa njia ya tafakari ya
kina. Haya ndiyo yaliyojionesha hata katika historia ya Kanisa. Waamini wanapaswa
kulitafakari, kulisali na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao.
Kwa vile
mwanadamu anaendelea kutopea katika dimbwi la dhambi, Mwenyezi Mungu kwa huruma na
upendo wake, ameamua kujinyenyekesha na kujishusha ili aweze kuwa karibu kabisa na
binadamu na hatimaye kumkomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huyu ndiye
Mungu ambaye yuko karibu katika historia na hija ya maisha ya mwanadamu, kama inavyojionesha
katika historia ya ukombozi. Amekuwa ni jirani yake ili aweze kumkomboa na wala si
kwa shuruti wala mikwara!
Baba Mtakatifu anasema, pale dhambi ilipoongezeka
maradufu, hapo pia neema na baraka za Mungu zimejionesha kwa kiasi kikubwa, ili kuweza
kuponya madonda ya dhambi kwa njia ya upendo na neema zake. Ndiyo maana Yesu alionesha
upendeleo wa pekee kwa wadhambi ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa
na mipaka, akitambua kwamba, wao kama wagonjwa walikuwa na uhitaji mkubwa wa tabibu
ambaye ndiye Yesu Kristo.
Hii ni changamoto kwa waamini kuendelea kumtegemea
Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, kwani Yeye ni mwingi wa huruma na
upendo.