Baraza la Maaskofu Katoliki Togo na changamoto zake!
Utume wa Mama Kanisa, ushuhuda amini wa imani na changamoto zinazolikabili Kanisa
ni kati ya mada zilizochambuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Togo katika mkutano
wake wa kawaida uliohitimishwa hivi katibuni huko Dapaong nchini Togo. Maaskofu wameangalia
kwa ukaribu zaidi maisha ya waamini wa Kanisa Katoliki wanaounda walau asilimia ishirini
ya idadi ya wananchi wote wa Togo na mchango wao katika ustawi na maendeleo endelevu
nchini humo.
Maaskofu kwa pamoja wamekubaliana kufanya mabadiliko makubwa
katika maisha ya Seminari, mahakama za Kanisa na Mafundisho ya Kanisa ili kuendana
na hali halisi pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Maaskofu wamechambua kwa kina na mapana hali
ya seminari kuu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Togo na
umuhimu wake kama kisima cha majiundo makini ya maisha ya kipadre na kitawa nchini
humo.
Maaskofu wameamua kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali,
Wazazi na Walimu ili kuhakikisha kwamba, wanafunzi nchini Togo wanapata elimu bora
wanapokua shuleni na kwamba, kuna haja kwa Kanisa kuchangia zaidi katika lengo hili.
Maaskofu wanayashukuru kwa namna ya pekee, Mashirika ya kitawa yanayoendelea kutoa
huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu kwa wananchi wote
wa Togo bila ubaguzi na kwamba, mikakati ya majiundo makini kwa vijana nchini humo
ni jambo linalowagusa sana.
Askofu mkuu Brian Udaigwe, Balozi wa Vatican nchini
Togo, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Togo. Katika mkutano
huu, aliwasilisha pia hati zake za utambulisho kutoka Vatican kwa Rais Faure Gnassinbe
wa Togo. kwa mara ya kwanza Askofu mkuu Brian aliweza kushiriki katika Maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na waamini wa Kanisa Katoliki nchini Togo. Amewapongeza
kwa mwamko na ari kubwa katika maisha yao ya Kikristo.
Askofu mkuu Brain amekazia
umuhimu kwa wananchi wa Togo kujikita tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili
katika mchakato unaopania ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani,
upendo na mshikamano wa dhati. Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha kwamba, anajenga
na kuimarisha utawala wa sheria, umoja wa kitaifa; msamaha na upatanisho; mambo msingi
katika ujenzi wa maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Togo linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwapatia mwakilishi
atakayewaonjesha upendo na mshikamano wa Baba Mtakatifu kwa wananchi wa Togo, hasa
wakati atakapokuwa anafanya hija za kichungaji kwenye Majimbo Katoliki nchini Togo.