Watanzania fanyeni kazi kwa juhudi na maarifa ili kuboresha maisha yenu!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Maisha
Bora kwa Watanzania hayawezi kuja kwa watu kushinda wanacheza mchezo wa pool badala
ya kujihangaisha kwa kufanya kazi na shughuli nyingine za kujiingizia mapato. Aidha,
Rais Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake itakomesha haraka iwezekanavyo kero ya wananchi
wa sehemu za Mkoa wa Njombe kulazimika kupanda mitini ili kupata mawasiliano ya simu
za mkononi.
Rais Kikwete ameyasema hayo Ijumaa, Oktoba 18, 2013, wakati alipohutubia
mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Wanginyi, Kata ya Lupembe, Wilaya ya Njombe katika
Mkoa Mpya wa Njombe kwenye siku yake ya kwanza katika ziara yake ya siku saba kukagua
na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa huo. Akizungumza na wakazi wa Kijiji hicho
na vijiji vya jirani, Rais Kikwete amezungumzia dhana nzima ya Maisha Bora kwa Watanzania
akisisitiza kuwa maendeleo na Maisha Bora kwa Kila Mtanzania hayawezi kupatikana kwa
watu kushinda wanacheza mchezo wa pool mchana kucha.
“Ndugu zangu, nimepata
kusema huko nyuma na nataka kurudia tena kuwa Maisha Bora kwa Kila Mtanzania yanawezekana
kwa watu kujituma na kuchapa kazi na siyo kwa watu kushinda kwenye meza za pool wakipiga
kale kampira huku wakiilaumu Serikali na kuulizana ‘Maisha Bora yako wapi’?” Ameongeza
Rais Kikwete: “Inawezekana kweli Maisha Bora yakaja kwa mtu anayeshinda anagonga mpira
wa pool kwenye meza? Ni kwa kufanya kazi kwa bidii na shughuli nyingine za kutuingizia
kipato ndipo maisha yetu yatakapokuwa bora.”
Kuhusu hali ya mawasiliano ya
simu Mkoani Njombe, Rais Kikwete, baada ya kuwa ameambiwa kuwa katika baadhi ya sehemu
za Mkoa huo, watu wanalazimika kupanda juu ya miti ili kupata mawasiliano, alisema
kuwa Serikali yake itakomesha haraka kero hiyo. “Ni ajabu na aibu kabisa kwamba watu
wanalazimika kupanda mitini ili kupata mawasiliano….Hii ni hatari … kwa sababu mtu
anaweza kuanguka na kuvunja viungo…mtu anaweza kuvunja kiuno,” alisema Rais Kikwete
huko watu wakiangua kicheko. “Tutahakikisha kuwa watu hawavunjiki viungo kwa sababu
ya kupiga ama kupokea simu za ndugu zao,” Rais Kikwete amewahakikishia wana-Njombe.
Katika
kufafanua azma hiyo ya Serikali kumaliza kero hiyo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali italimaliza
tatizo la mawasiliano katika Mkoa wa Njombe kwa awamu mbili. Alisema kuwa katika awamu
ya kwanza, kiasi cha Sh.milioni 260 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha mawasiliano
katika vijiji 25 vya Jimbo la Uchaguzi la Njombe Kaskazini na kuwa kazi hiyo itakuwa
imekamilika ifikapo Machi, mwakani, 2014. “Tunataka watu waache kupanda kwenye miti
kwa kutafuta mawasiliano ya simu tu.”
Amesema kuwa katika awamu ya pili, kiasi
cha Sh.bilioni 1.552 zitatumika kutoka Mfuko wa Mawasiliano Vijijini kwa ajili ya
kuboresha mawasiliano ya simu katika Mkoa mzima wa Njombe. Amesema kuwa kazi ya kuboresha
mawasiliano katika awamu hiyo ya pili, itakamilika ifikapo Agosti, mwakani, 2014.
Kuhusu
matumizi ya simu zenyewe, Mheshimiwa Mbarawa amewataka Watanzania kuzitumia simu hizo
za mkononi vizuri kwa mawasiliano ya maana na yasiyokuwa ya ovyo ikiwa ni pamoja na
kutukana watu. “Tuzitumie simu zetu vizuri kwa mawasiliano mazuri na ya maana na siyo
kutumia simu kujenga na kusambaza fitina na majungu ama kushiriki matusi dhidi ya
watu wengine.”