2013-10-21 14:17:04

Tangazeni Injili ya Upatanisho kwa kukoleza mchakato wa upatanisho miongoni mwa Wakristo


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 21 Oktoba 2013 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani pamoja na Tume ya Kimataifa kati ya Waluteri na Wakatoliki, waliomtembelea mjini Vatican. Amewashukuru kwa kushiriki katika sherehe ya kuanza utume wake kama Askofu wa Jimbo kuu la Roma na kwamba, Makanisa haya mawili katika kipindi cha miaka kumi yamepiga hatua kubwa katika majadiliano ya kiekumene pamoja na kudumisha ushirikiano wa kidugu.

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kiekumene katika maisha ya kiroho ni kiini cha umoja kamili miongoni mwa wafuasi wa Kristo; mchakato unaopaswa kufanywa kwa moyo wa unyenyekevu ili kuweza hatimaye, kuufikia umoja kamili. Majadiliano ya kitaalimungu kwa mwaka huu yameingia katika Mwaka wa 50 tangu yalipoanzishwa.

Maadhimisho ya Majadiliano ya kiekumene kati ya Waluteri na Wakatoliki kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Miaka 500 ya mageuzi ya Kiluteri yanaongozwa na kauli mbiu "kutoka katika kinzani kuelekea kwenye umoja. Tafsiri ya Mabadiliko kati ya Waluteri na Wakatoliki kwa Mwaka 2017". Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Makanisa haya mawili kujikita katika majadiliano ya kiekumene mintarafu historia, matokeo na majibu yaliyotolewa kwa nyakati tofauti.

Uwe ni muda wa kuombana msamaha kutokana na kinzani zilizojitokeza miongoni mwa waamini wa Makanisa haya mawili mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa pamoja waanze mchakato wa furaha kuelekea umoja kamili ambao umefunuliwa ndani ya mioyo yao, huku wakiangalia mbele kwa matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, miaka kumi iliyopita kimekuwa ni kipindi ambacho ushuhuda wa udugu kati ya Waluteri na Wakatoliki umejionesha, kielelezo cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene na umoja kamili katika medani mbali mbali za maisha.

Magumu na changamoto zitaendelea bado kujitokeza, mambo yanayohitaji kwa namna ya pekee: uvumilivu, majadiliano na hali ya kuelewana bila kushika tama kwani umoja miongoni mwa Wakristo si juhudi binafsi bali ni kazi ya Roho Mtakatifu, ambaye anawachangamotisha waamini kufungua akili na mioyo yao kwa imani ili aweze kuwaonesha njia ya upatanisho na umoja.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili anaendelea kuwaalika Wakristo wote kutangaza Injili ya Upatanisho kwa kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa Upatanisho miongoni mwa Wakristo. Jambo hili linawezekana anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa maisha ya sala na majadiliano; upyaisho wa maisha na wongofu wa ndani, ili kuweza kupokea msaada unaotoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ili kutekeleza mwaliko wa Kristo kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja!







All the contents on this site are copyrighted ©.