Sinodi maalum kuhusu Familia hapo 2014 inapania kuangalia changamoto za familia katika
shughuli za kichungaji!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Bikira Maria katika Mwaka wa
Imani, amewataka wanandoa na familia kuhakikisha kwamba, wanamwilisha maneno makuu
matatu katika maisha yao ya kila siku: Maneno haya ni: Tafadhali, Sahamani na Asante.
“Changamoto
za familia kichungaji katika Uinjilishaji” ndiyo kauli mbiu itakayoongoza Maadhimisho
ya Sinodi Maalum kwa ajili ya familia, itakayofanyika kuanzia tarehe 5 hadi tarehe
19 Oktoba, 2014.
Nia ya Baba Mtakatifu Francisko kwa kutangaza Maadhimisho
ya Sinodi Maalum kwa Ajili ya Familia mwezi Oktoba 2014 inapania pamoja na mambo mengine
kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu dhamana n anafasi
ya familia katika maisha na utume wa Kanisa. Huu utakuwa ni muda muafaka wa Kanisa
kama Jumuiya ya waamini kusali na kufanya tafakari ya kina kuhusu familia.
Hii
ni Sinodi itakayowahusisha viongozi wakuu wa Kanisa pamoja na wajumbe kutoka katika
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia. Ni ufafanuzi
uliotolewa hivi karibuni na Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican wakati
akifafanua kwa kina, uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuitisha Sinodi Maalum
kwa ajili ya Familia, taasisi ambayo ni msingi wa Kanisa na Jamii, lakini inayokabiliana
na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake.
Padre Federico Lombardi
anasema, huu ni mwelekeo sahihi kwamba, Kanisa, liweze kutembea kwa pamoja katika
mikakati ya kichungaji mintarafu utume na maisha ya familia, chini ya usimamizi na
uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro akisaidiana na Maaskofu wenzake katika kutekeleza
dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Sinodi itagusia mambo
msingi yanayopaswa kushughulikiwa na Kanisa katika ujumla wake.
Ufumbuzi wa
changamoto na fursa mbali mbali kuhusu utume na maisha ya familia utaendelea kutekelezwa
na wadau mbali mbali kila mtu kadiri ya wajibu na dhamana yake, ili kuondokana na
mkanganyiko unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mafundisho ya Kanisa kuhusu
familia. Lengo la Baba Mtakatifu Francisko ni kuhakikisha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu
Petro, Maaskofu pamoja na Makanisa mahalia yanashikamana katika kulinda na kutetea
tunu msingi za maisha ya familia.