2013-10-21 09:54:50

Sekondari 150 nchini Tanzania kupata mafunzo kwa njia ya mtandao wa mawasiliano!


Kampuni ya Huawei ya China ina mpango wa kuzisaidia shule za sekondari 150 nchini Tanzania ili ziwe zikipata mafunzo kwa njia ya mtandao wa mawasiliano (E-Education) kama njia ya kukabiliana na uhaba wa walimu na vitabu vya masomo. Hayo yameelezwa Jumapili, Oktoba 20, 2013 na Rais wa Kampuni hiyo, Bw. William Xu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye makao makuu yao jijini Shenzhen, China.

Alisema walipokea maombi ya Serikali ili kuona jinsi mkongo wa mawasiliano ya Taifa (NCITBB) utakavyoweza kuinua kiwango cha elimu ya watoto wa Kitanzania kwa kiasi kikubwa. Kampuni ya Huawei ndiyo iliyojejenga mkongo huo. Alisema kwa kuanzia mradi huo utazihusu shule 50 ambapo shule mbili kutoka kila mkoa zitaunganishwa kwenye mtandao saa zote (ziko online) zikiwa na madarasa ya kujifunzia teknolojia mpya (multimedia classrooms), maabara ya kompyuta (computer lab), projekta, mafunzo ya kwenye mtandao yanayofundishwa kwa njia ya video, (Online video teaching) na (online applications).

“Shule nyingine 100 zimekwishaainishwa lakini zenyewe zitakuwa zikipata mafunzo offline (hazitakuwa mtandaoni moja kwa moja), bali katika awanu ya pili zinaweza kuunganishwa na kuwa online kutegemea na upatikanaji wa intaneti na kasi yake,” alisema. Alisema shule hizi zitakuwa zikipokea mawasiliano kutoka kituo chao kikuu ambacho kimejengwa Dakawa, Morogoro.

Vilevile Bw. Xu alimkabidhi Waziri Mkuu hati ya makabidhiano ya msaada wa dola za marekani 155,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na vifaa vya komputa kwa shule ya msingi Kibaoni ambayo alisoma Waziri Mkuu iliyoko wilayani Mlele, Katavi.

Akitangaza matumizi ya msaada huo, mtaalamu kutoka kampuni ya Huawei, Bw. Moses Hella alisema msaada huo utatumika kujenga madarasa mawili moja likiwa computer lab na jingine ni darasa la kujifunzia teknolojia mpya (multimedia classroom), kompyuta 50, laptop tano kwa ajili ya walimu, Huawei tablets 100 na audio system.

Kwa upande wake, Waziri Mku aliishukuru kampuni hiyo kwa kukubali kutumia teknolojia yake katika kuendeleza elimu nchini kwa kuanzisha mfumo wa E-Education kwenye shule 50 kwa wakati mmoja. Aliishukuru pia kampuni hiyo kwa kukisaidia Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela cha Arusha na kuongeza kuwa angependa kuona chuo hicho kinakuwa cha mfano katika maeneo ya utafiti na teknolojia ya mawasiliano barani Afrika.

Kuhusu msaada kwa shule ya msingi Kibaoni, Waziri Mkuu aliwashukuru kwa kumuunga mkono katika kampeni yake ya kuhakikisha amefanya kitu kuisaidia shule hiyo ambayo alisoma kati ya mwaka 1957 na 1960. “Ninawashukuru sana kwa msaada huu. Niliahidi kwamba kabla sijaondoka madarakani nataka nifanye jambo la ukumbusho kwa manufaa ya jamii ya eneo lile. Kwa kweli nawashukuru sana kwa kutupatia msaada huu naamini kuwa shule hii sasa ni ya kisasa na wanafunzi wake watakuwa na elimu ya teknohama na siyo wa BBC (born before computers) kama mimi.
Alisema ataikabidhi hati hiyo kwa viongozi wa Halmashauri yake ili watunze kwenye rekodi zao. Shule ya msingi Kibaoni aliyosoma imechakaa, eneo ilipo ni dogo sana na haifai kwa ukarabati. Ili kukamilisha azma yake, Waziri Mkuu aliomba Halmashauri ya Wilaya ya Mlele itafute eneo jipya ili ujenzi wa shule hiyo ukikamilika, wanafunzi walioko katika shule hiyo wahamie kwenye shule mpya. Hadi sasa madarasa 12 yamekwishajengwa na kuezekwa. Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China.








All the contents on this site are copyrighted ©.