Miaka 30 ya Kituo cha Televisheni cha Vatican si haba!
Kituo cha Televisheni cha Vatican, kinaadhimisha Miaka 30 tangu kilipozinduliwa na
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa katika kutoa
kipaumbele kwa mwanadamu aliyeumba kwa sura na mfano wa Mungu; umuhimu wa kusimama
kidete kulinda na kutetea haki na amani, pamoja na kuwajengea watu matumaini kwa leo
na kesho iliyo bora zaidi.
Kituo hiki kimeendelea kusoma alama za nyakati
katika mabadiliko yanayojitokeza katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu;
daima kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika uwajibikaji. Haya ni kati ya mambo ambayo
yameendelea kufanyiwa kazi na Kituo cha Televisheni cha Vatican katika utekelezaji
wa majukumu yake ya kutoa picha za televisheni kwa vituo mbali mbali vya televisheni
duniani.
Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Rais Giorgio Napolitano wa Italia
kwenda kwa Monsinyo Dario Edoardo ViganĂ², mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha
Vatican katika maadhimisho ya Miaka 30 ya Kituo hicho. Sherehe hizi zimehudhuriwa
na wadau mbali mbali katika sekta ya mawasiliano ya jamii ndani na nje ya Italia.
Ilikuwa ni fursa kwa wadau hawa kufanya majadiliano ya kina kuhusu mada mbali mbali
zinazogusa uwanja wa mawasiliano ya kijamii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia.
Vatican imekuwa ni mdau mkubwa wa mawasiliano ya
jamii, kwani itakumbukwa kwamba, Gazeti la L'Osservatore Romano linalomilikiwa na
kuendeshwa na Vatican limekwisha timiza miaka 150 tangu lilipoanzishwa na Radio Vatican
hivi karibuni imeadhimisha Miaka 80 tangu ilipoanzishwa, matukio yote haya si haba
anasema Rais Napolitano katika ulimwengu wa upashanaji habari.
Kituo cha Televisheni
cha Vatican kimekuwa mstari wa mbele kwa kuonesha maisha na utume wa viongozi wakuu
wa Kanisa walioko mjini Vatican; matukio ambayo yanatendeka kila kukicha. Ni kwa njia
ya kituo hiki kwamba, mamillioni ya watu waliweza kumfahamu Mwenyeheri Yohane Paulo
wa Pili katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa.
Ni kituo ambacho kimefuatilia
kwa umakini mkubwa mikutano ya uchaguzi wa Mapapa katika kipindi cha miaka thelathini
iliyopita, lakini kwa umahiri na ufanisi mkubwa wakati wa uchaguzi wa Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko.
Rais Giorgio Napolitano anakipongeza
Kituo cha Televisheni cha Vatican kwa kusoma alama za nyakati na kwenda na wakati
katika mabadiliko ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari duniani. Anawatakia
kheri na baraka tele katika utume wao kwenye ulimwengu wa mawasiliano ya Jamii.