2013-10-21 14:45:38

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani Jimbo Katoliki Zanzibar!


Jimbo Katoliki la Zanzibar limeadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu imani Katoliki iingie katika visiwa hivyo. Adhimisho hili limefanyika Jumamosi, tarehe19 Oktoba 2013. Tukio hili la kihistoria limeanza kusherehekewa kwa kufunguliwa rasmi shule iliyoanzishwa na Jimbo: Francis Maria Paul Libermann School.

Padri Francis Maria Paul Libermann ni mwasisi wa Shirika la Mapadri Mapadri wa Roho Mtakatifu (The Spiritans) ambao walihusika na upandaji wa mbegu ya imani katika visiwa hivi. Pd. Francis alifanya jitihada za pekee kuwakomboa watumwa, na kuwapatia elimu, kwani aliamini kwamba “Elimu ni ufunguo wa maisha, kumwezesha mtu kupata uhuru wa kweli.”

Mgeni rasmi katika Jubilei hii na ufunguzi wa shule na mahafari kwa wanafunzi wa chekechea, msingi na sekondari alikuwa ni Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika nasaha zake alisisitiza juu ya umuhimu wa elimu. Kwani elimu si tu inamkomboa mwanadamu kutoka katika ujinga na imani potofu, lakini pia ni kiungo thabiti cha upendo, amani ustawi na mshikamano katika jamii. Kardinali Pengo asisitiza kuwa elimu inafukuza dhana ya kudhaniana vibaya, inafukuza chuki kati ya watu, inafukuza uadui; kwani yenyewe ni nuru kati ya wanajamii.

Askofu Augustino Ndeliakyama Shao katika adhimisho hili, alisisitiza umuhimu wa elimu. Alitanabaisha kwamba, Kanisa linatoa elimu si kwa lengo la kidini, lakini kwa lengo la kumnyanyua mwanadamu toka katika tope la ujinga, ambalo ni adui mkubwa wa maendeleo ya watu. Alimshukuru Mwadhama Kardinali Pengo kwa kutenga muda wake na kushirikiana nao katika tukio hilo adhimu.

Shule ya Francis Maria Paul Libermann, ipo katika Shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kiasi cha kilomita 10 kusini mwa Mji Mkongwe Zanzibar. Inajumuisha shule ya chekechea, shule ya msingi na shule ya sekondari (kidato 1-4). Ilianza kujengwa mwaka 1994.

Shule hii ina changamoto mbalimbali, hasa upatikanaji wa idadi ya kutosha ya wanafunzi kwa madarasa yote, tatizo la kulipa ada kwa wakati, upatikanaji wa walimu wa kutosha na wenye sifa sitahiki, majirani wanaozunguka shule kutoelewa malengo ya shule hiyo na hivyo kutokuwa tayari kuwapeleka watoto wao hapo shuleni kupata elimu na umuhimu wa kuwepo kwa amani.

Sherehe ilihudhuriwa na mapadri, watawa na wazazi wa wanafunzi na ilipambwa na shamrashamra mbalimbali ikiwemo kubariki jiwe na msingi na udungo wa shule hiyo, pamoja na shangwe mbalimbali za kitamaduni zilizofanywa na wanafunzi wenyewe: utenzi, nyimbo za kiswahili na kifaransa na ngoma. Ngoma ya kibati yenye asili ya kisiwa cha Pemba ilitia fora.

Mwishoni, Mwadhama aliwaahidi kurudi tena pamoja na maaskofu wote, au angalau wa metropolitani ya Dar es Salaam, kuja kumshukuru Mungu pamoja nao, kwani Zanzibar ndilo lango la imani ya Afrika Mashariki yote, Jubilei yao, ni jubilei ya Afrika’ Mashariki nzima.








All the contents on this site are copyrighted ©.